Maafisa Waandikishaji waaswa uadilifu
Na. Faraja Mbise, DODOMA
Maafisa waandikishaji orodha ya wapiga kura
uchaguzi wa serikali za mitaa mwaka 2024 Halmashauri ya Jiji la Dodoma wameaswa
kuwa waadilifu ili Dodoma iwe ya kwanza kwa idadi kubwa ya watu walioandikishwa.
Mjumbe wa Kamati ya Uratibu wa Uchaguzi wa Serikali za Mitaa Mkoa wa Dodoma, Coletha Kiwale
Hayo yalisemwa na Mjumbe wa Kamati ya Uratibu
wa Uchaguzi wa Serikali za Mitaa Mkoa wa Dodoma, Coletha Kiwale wakati
akizungumza na maafisa waandikishaji, watendaji wa mitaa, wasimamizi wasaidizi
ngazi ya kata pamoja na maafisa watendaji wa kata wakati wa mafunzo kwa maafisa
waandikishaji wa orodha ya wapiga kura leo katika ukumbi wa Mtumba Complex
jijini Dodoma.
Kiwale aliwataka maafisa waandikishaji kuwa
weledi na wenye ufanisi katika suala la muda, mavazi na utoaji taarifa kwa wakati.
Msisitizo mwingine alisisitiza wawe waadilifu na wahamasishaji kwa
waandikishaji kujitokeza kwa wingi katika kujiandikisha kwenye orodha ya wapiga
kura.
“Napenda tushirikishane tunapoelekea kwenye Uchaguzi
wa Serikali za Mitaa, tungependa kuwaambia mambo ya kuzingatia mambo yafuatayo:
moja, muda wa kufungua vituo na kufunga vituo. Pili, Tunawaomba maafisa uandikishaji
kuwa wahamasishaji wa watu kuja kujiandikisha, pamoja na familia zao kwasababu Mkuu
wa Mkoa wa Dodoma anatamani Dodoma iongoze kwa idadi kubwa ya watu watakaokuwa
wamejiandikisha kwenye orodha ya daftari nchi nzima, kutoa taarifa za uandikishaji
mpaka inapofika saa moja na nusu jioni kwa kufuata muundo wa kitaasisi. Maafisa
waandikishaji kuripoti kwa Afisa Mtendaji wa Mtaa. Pia hatutarajii Afisa
Mwandikishaji kutafutwa kwenye simu na asipatikane” alisisitiza Kiwale.
Kwa upande wake CPA. Eric Ntikahera, aliwataka
maafisa waandikishaji kufanya mambo muhimu tu yanayohusu zoezi la uandikishaji.
Aliwataka wafuate maadili na kanuni za utumishi na uadilifu pindi wawapo katika
vituo vya kujiandikisha. Vilevile, aliwataka wasigeuze vituo hivyo kama sehemu
ya starehe bali waheshimu vituo hivyo vya kuandikishia kama wanavyoheshimu sehemu
nyingine za kazi.
“Mwaka 2019 tulifundisha maafisa waandikishaji
wakaelewa, lakini nafikiri ilikuwa vitu viwili tofauti, mtu kapewa elfu kumi
yake ya chakula yeye kanunua bia nne pembeni, yaani uandikishaji unaendelea na
ulevi unaendelea. Kwahiyo, kimsingi tijiepushe katika vitu vitakavyokwamisha
hili zoezi” alisema CPA. Ntikahera.
Wakati huohuo, Afisa Uchaguzi Halmashauri ya
Jiji la Dodoma, Albert Kasoga alipokea salamu hizo kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa
wa Dodoma na kuahidi utekelezaji katika zoezi la uandikishaji orodha wa wapiga
kura kwa weledi.
“Tunamuahidi Mkuu wa Mkoa wa Dodoma
kutekeleza yale aliyoagiza ili Dodoma iwe ya kwanza katika zoezi la uandikishaji
kwenye orodha ya wapiga kura katika Uchaguzi
wa Serikali za Mitaa nchi nzima” alisema Kasoga.
Ikumbukwe kuwa zoezi hilo la uandikishaji wa
orodha ya wapiga kura halitahusisha uwepo wa kadi au kitambulisho cha mpiga
kura, ilimradi tu mwananchi awe amejiandikisha katika orodha ya wapiga kura,
vitambulisho vitakavyohusika ni leseni ya udereva, kadi ya Bima ya Afya, kitambulisho
cha kazi au kitambulisho cha Taifa (NIDA). Iwapo mwananchi hana atatambulishwa
na jirani yake wa mtaa husika.
MWISHO
Comments
Post a Comment