Mradi wa majaribio wa usimamizi taka kuanza Dodoma
Na. Asteria Frank, DODOMA
Halmashauri ya Jiji la Dodoma kwa kushirikiana
na Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira wanatekeleza mradi wa
majaribio wa usimamizi wa taka za plastiki katika Jiji la Dodoma kwa lengo la
kuhamasisha njia bunifu katika usimamizi wa taka za plastiki kupitia dhana ya
uchumi rejeshi ili kupunguza taka za plastiki kwenye mazingira na kuboresha
maisha na uchumi wa taifakwa ujumla.
Baada ya kutembelea na kukagua
maendeleo ya mradi huo uliopo katika Kata ya Chamwino, Afisa Mazingira wa Halmashauri
ya Jiji la Dodoma, Aliy Mfinanga, alisema kuwa mradi wa majaribio utawanufaisha
na kuwawezesha jamii na vikundi vya usafi kufanya shughuli za ukusanyaji na
usafirishaji wa taka katika Kata ya Chamwino kwa nia ya kutia thamani kupitia dhana
ya uchumi rejeshi ili kutunza Mazingira kutokana na plastiki.
“Tumeshazoea kuona msisitizo mkubwa
kuwa taka ni taka na kwamba haifai tena, lakini kupitia mradi huu wa majaribio
tunataka kuonesha jamii kuwa tunaweza kuongeza thamani ya taka kutokana na
plastiki ili kuweza kufanya dhana nzima ya uchumi rejeshi” alisema Mfinanga.
Alisema kuwa wanategemea kuwa na
mashine ambayo itatumika kusaga chupa za plastiki ambazo zitakuwa zimetoka
mtaani, kwenye makazi, masoko, maeneo ya biashara na kwenye taasisi sehemu
ambapo vikundi hivi vya Kata ya Chamwino vinafanya kazi.
“Lengo letu ni kusaga chupa za plastiki
na kuzisafirisha kwenda Dar-es-Salaam kwaajili ya kutengeneza bidhaa nyingine
za plastiki ikiwa ni pamoja na vyombo vya plastiki kama vifaa vya umeme, samani
na kadhalika. Kwahiyo, kupitia mradi huu wa majaribio tunafanya kwenye ngazi ya
vikundi na tutaufanya muda wa majaribio ili tuweze kuona namna gani tunaweza
kuu ‘upscale’ kulingana na lengo tulilojiwekea”.
“Tunatarajia pia uchumi wa vikundi
vinavyo fanya shughuli hii kupanda kidogo kwasababu kwa sasa wanafanyakazi ya
kukusanya na kusafirisha taka. Lakini kupitia mradi huu wa majaribio wa
usimamizi wa taka za plastiki wanaenda kujiongezea kipato kwasababu kilo ya
chupa sasa hivi inauzwa shilingi 300 wenyewe kwakuwa wanafanya hii kazi
inamaanisha watakuwa wanapata ‘material free of charge’ na baada ya kusaga
tunategemea kulingana na soko la sasa ni kuanzia shilingi 800 mpaka 1,200 na
mashine yetu kwa siku inaweza kusaga nusu tani ambazo ni takribani kilo 500” alisema
Mfinanga.
MWISHO
Comments
Post a Comment