Hakuna Mamluki yeyote atakayeandikishwa kwenye orodha ya wapiga kura Jiji la Dodoma
Na. Faraja Mbise, DODOMA
Msimamizi
wa Uchaguzi Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Dkt. Frederick Sagamiko amekanusha
taarifa zinazosambaa katika mitandao ya kijamii kuhusu mwenendo wa uandikishaji
kuwa wanaandikishwa mamluki kwenye orodha ya wapiga kura.
Msimamizi wa Uchaguzi Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Dkt. Frederick Sagamiko akifafanua mwenendo wa zoezi la uandikishaji orodha ya wapiga kura Jiji la Dodoma
Kanusho
hilo alilitoa ofisini kwake alipokuwa akiongea na waandishi wa habari kufuatia
tuhuma zilizotolewa na Chama cha Demokrasia na Maendeleo Chadema kuhusu mwenendo
wa uandikishaji orodha ya wapiga kura unaoendelea wakidai kuwa kituo kimoja
kiliandikisha watu kinyume na utaratibu.
Dkt.
Sagamiko alisema “kutokana na taarifa zilizosambaa katika mitandao ya kijamii,
zinazoelezea kuhusu muenendo wa uandikishaji katika Halmashauri ya Jiji la
Dodoma kwa bahati mbaya sana taarifa ile inaelezea kuhusu mwenendo mbaya wa
uandikishaji. Baada ya kupitia na kusikiliza kwa makini video ile, nikabaini
kwamba tatizo sio mwenendo wa uandikishaji, bali tatizo ni uelewa mdogo juu ya
kanuni na miongozo inayotumika katika uendeshaji wa Uchaguzi wa Serikali za
Mitaa mwaka huu 2024”.
Msimamizi
huyo alifafanua kuwa wanaoruhusiwa kuandikisha katika orodha ya wapiga kura ni
maafisa waandikishaji waliochaguliwa na Msimamizi wa Uchaguzi, kushiriki katika
kuandika taarifa za mpiga kura. “Kwenye kituo, nje ya mwandikishaji na wakala
wa chama, wapo baadhi ya watu walioruhusiwa kikanuni kama Msimamizi wa Uchaguzi,
kuhakikisha anatimiza wajibu wake na kwenda kufanya ukaguzi mwingine. Lakini
hakuna mtu mwingine anaeruhusiwa kuwa kwenye kituo cha kujiandikishia”
alisisitiza Dkt. Sagamiko.
Msimamizi
huyo alisema kuwa Halmashauri ya Jiji la Dodoma ina jumla ya vituo 666 vya
kujiandikishia wapiga kura na vyama vya siasa vimeruhusiwa kuweka mawakala wao
katika kila kituo. “Kwa sisi Halmashauri ya Jiji la Dodoma tuna jumla ya vituo 666,
na nchi yetu tuna vyama vya siasa takribani 19 vyenye usajili wa kudumu na sisi
tunaamini vyote hivyo vinashiriki katika uchaguzi huu. Halmashauri tulifuata
taratibu zote kuwaarifu vyama kuweza kuweka mawakala wakati huu wa
kujiandikisha. Naomba nichukue nafasi hii kuwataarifu kwamba ni vyama viwili tu
vilivyofanikiwa kuweka mawakala, Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimefanikiwa kuweka
mawakala 666 katika kila kituo na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) wamefanikiwa
kuweka mawakala 55. Kwa kuwa malalamiko yale yametolewa na viongozi CHADEMA, naomba
kutoa taarifa kuwa CHADEMA wamefanikiwa kuweka mawakala katika kata sita, kati
ya kata 41 zilizopo Halmashauri ya Jiji la Dodoma. Kata hizo ni Kikombo (9),
Kikuyu Kaskazini (12), Chamwino (7), Chihanga (4), Ng’hong’onha (19) na Mbabala
(4). Lakini kwa bahati mbaya eneo ambalo limeripotiwa matukio kutokea hakuna
mawakala wa CHADEMA waliowekwa” alisema Dkt. Sagamiko kwa mshangao.
Kamati ya Usimamizi wa Uchaguzi wa Serikali za Mitaa Halmashauri ya Jiji la Dodoma
Msimamizi
huyo alivitaka vyama vya siasa kufuata kanuni na miongozo ya Uchaguzi wa Serikali
za Mitaa ili uchaguzi uwe wa huru na wa demokrasia. “Nitoe rai kwa viongozi wa
vyama vya siasa kutokushiriki katika uvunjifu wa amani katika maeneo yetu ya vituo
na wazingatie kanuni na kwa bahati nzuri walishagawiwa kanuni” aliongea kwa msisitizo
Dkt. Sagamiko.
Wakati
huohuo, aliwataka wananchi wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma wenye sifa za kujiandikisha
kujitokeza na kujiandikisha kwenye orodha ya wapiga kura ili waweze kuchagua
viongozi wa Serikali za Mitaa. Aliwahakikishia kuwa hakuna mtu wa kuwapora haki
hiyo. Aliwakumbusha sifa za kujiandikisha katika orodha ya wapiga kura ni kuwa
mtanzania, mwenye umri wa miaka 18 na kuendelea, mkazi wa kijiji, kitongoji au
mtaa ambao uchaguzi unafanyika na uwe na akili timamu.
Akiongelea
umuhimu wa waandishi wa habari na vyombo vya habari, alisema kuwa ni wadau
muhimu katika kutoa elimu na hamasa kwa wananchi. “Kwakuwa ninyi ni wadau
muhimu, mnapaswa kuzielewa kanuni hizi. Naomba niwakabidhi kanuni hizi na
ninawaomba mzisome na pale mtu yeyote atakapoitwa kwenye ‘press’, mpitie
muongozo wa uchaguzi kabla hamjaenda kutoa taarifa ili muweze kujiridhisha kama
huyo mtu ameongea kwa mujibu wa kanuni au la” alisema Dkt. Sagamiko.
Ratiba
ya shughuli za uchaguzi wa serikali za mitaa inaonesha kuwa zoezi la
uandikishaji katika orodha ya wapiga kura lilianza tarehe 11 Oktoba, 2024
litamalizika tarehe 20 Oktoba, 2024.
MWISHO
Comments
Post a Comment