Gari la Darasa Tembezi latoa elimu Mitaa ya Jiji la Dodoma
Na. Asteria Frank, DODOMA
Gari la Darasa Tembezi kutoka Halmashauri
ya Jiji Dodoma linalopakia abiria kwa lengo la kuelimisha kuhusu uandikishaji wa
orodha ya wapiga kura kuelelea Uchaguzi wa Serikali za Mitaa linaendelea
kuwafikia wananchi wengi katika maeneo mbalimbali ya halmashauri.
Darasa Tembezi linapita kwenye kila kituo likipakia abiria na kuwapa elimu kisha linawashusha katika vituo vyao kwa kuhakikisha wameelewa zoezi la kujiandikisha katika orodha ya mpiga kura zoezi lililoanza tarehe 11-20 Oktoba, 2024 kuelekea Uchaguzi wa Serikali Mitaa.
Muelimishaji na muhamasishaji wa Darasa Tembezi,
Isabella Bruno aliwaeleza abira kuwa kuelekea Uchaguzi wa Serikali za Mitaa
utakaofanyika tarehe 27 Novemba, 2024 na kusema kuwa mwananchi wanatakiwa
kujiandikisha kwenye orodha ya wapiga kura katika vituo vilivyopo katika ofisi
za mitaa, shule za msingi na sekondari, zahanati na vituo vya afya, maeneo ya
wazi yenye mikusanyiko ya watu na majengo mengine ya taasisi za umma yaliyopo
katika mitaa au vitongoji ili aweze kushiriki kuchagua mwenyeki pamoja na
wajumbe wa kamati ya utekelezaji.
Alisema kuwa kuna utofauti kati ya
kujiandikisha katika daftari la kudumu la mpiga kura ambalo liliwawezesha
wananchi kupata kadi ya kupigia kura mwaka 2025 kwenye kuchagua diwani, mbunge
na raisi. Kujiandikisha kwenye orodha ya wapiga kura ni kwaajili ya kupata sifa
ya kushiriki Uchaguzi wa Serikali za Mitaa na linabeba orodha ya wananchi
wanaoishi katika eneo husika pekee.
“Zoezi la kujiandikisha kwenye daftari la
kudumu la mpiga kura haliusiani kabisa na Uchaguzi wa Serikaliza Mitaa. Kwahiyo,
ili kupata sifa ya kushiriki Uchaguzi wa Serikari za Mitaa ni lazima
ujiandikishe kwenye orodha ya wapiga kura katika mitaa tunayotoka” alisema
Bruno.
Aliongeza kuwa kupata sifa ya kushiriki Uchaguzi
wa Serikali za Mitaa ni lazima awe raia wa Tanzania, mwenye umri wa miaka 18 na
kuendelea, na mkazi wa mtaa ambao uchaguzi unafanyika. Pia awe na akili timamu
na awe amejiandikisha kupiga kura katika mitaa husika na zoezi la kujiandikisha
ni la muda mfupi.
Balozi wa kupinga Rushwa, Noela Maginga alisema
kuwa ruswa ni kitendo cha kutoa au kupokea kitu chenye thamani bila kufuata
taratibu au kwenda kinyume na sheria. Hivyo, kuelekea Uchaguzi wa Serikali za Mitaa
na hata uchaguzi ujao mwakani vitendo vya rushwa havitakiwi kuchukua nafasi
ikiwemo rushwa ya ngono.
“Mimi kama Balozi wa kupinga rushwa
napenda kuwakataza msipokee wala msikubali kuchukuwa rushwa na kama unaweza
kukutana na tatizo kama hilo unawza kupiga namba 113 kwaajili ya kuripoti ukiwa
na ushahidi asanteni na ninawaomba mshiriki katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa”
alisema Maginga.
Abiria wa gari la Darasa Tembezi, Aliy
Mhagama alisema kuwa amefurahia kupata elimu kuhusu swala zima la Uchaguzi wa
Serikali za Mitaa na kupewa utofauti kati ya daftari la kudumu la mpiga kura na
orodha ya wapiga kura.
“Mimi kama kijana nawahusia na nina
wakumbusha vijana wenzangu kuwa jambo la Serikali za Mitaa ni la zuri sana na
limeidhinishwa na katiba ya nchi yetu. Kwahiyo, ni vema sisi sote kushiriki ili
tuweze kuchagua viongozi bora na walio sahihi na ambao wanaweza kuja kutuletea mabadiliko.
Hivyo, vijana wenzangu tusibaki nyuma twende tukajiandikishe kwenye orodha ya
wapiga kura” alisema Mhagama.
MWISHO
Comments
Post a Comment