MRADI WA UBORESHAJI USALAMA WA MILKI ZA ARDHI WACHANGIA ONGEZEKO LA WANAWAKE KUMILIKI ARDHI NCHINI
Na Eleuteri Mangi WANMM
Mradi wa Uboreshaji Usalama wa Milki za Ardhi (LTIP)
unaotekelezwa na Serikali kwa kushirikiana na Benki ya Dunia umeongeza idadi ya
wanawake wanaomiliki ardhi nchini kutoka asilimia 25 hadi 35 hatua inayosaidia
kuinua kiuchumi wao na taifa kwa ujumla.
Kauli hiyo imetolewa na Mratibu Mradi LTIP Bw. Joseph Shewiyo
unaotekelezwa chini ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi wakati
akifungua kikao kazi cha Asasi za kiraia kujadili utekelezaji wa mradi huo
Januari 16, 2024 jijini Dodoma.
"Mna jukumu kubwa, mnapaswa kuongeza wigo katika kutekeleza
majukumu yenu kufanikisha kutoa hati milki za kimila ili kuinua uchumi wa
wananchi, mna mchango mkubwa kwa ongezeko la wanawake wanaomiliki ardhi kutoka
asilimia 25 hadi 35, mkafanye kazi yenu kwa weledi msiharibu ndoa za watu"
amesema Bw. Shewiyo.
Mradi huo unaotekelezwa na Serikali kupitia Wizara ya Ardhi,
Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa kushirikiana na Benki ya Dunia unalenga
kuimarisha mifumo ya utawala wa ardhi, kuongeza usalama wa milki za ardhi kwa
wanaume na wanawake na hivyo kukuza uwekezaji wa ardhi nchini.
Majukumu yanayotekelezwa katika mradi huo ni pamoja na kuongeza
usalama wa milki za ardhi kwa kupanga, kupima na kumilikisha wananchi ardhi
mijini na vijijini, kuboresha mifumo ya usimamizi wa taarifa za ardhi nchini,
kuimarisha usimamizi na ufuatiliaji wa mradi.
Aidha, Asasi za Kiraia katika mradi huo zinajukumu la kutoa
elimu kwa Jamii kuhusiana na mradi, kutoa elimu kwa makundi maalumu kama vile
wanawake, wazee, watoto na watu wenye ulemavu kuhusu haki zao katika umiliki wa
ardhi, kushiriki katika utatuzi wa migogoro ya Ardhi, kutoa ushauri wa namna ya
kushugulikiamasuala ya Jamii na mazingira yanahusu mradi, kushirikiana na timu
ya mradi katika kuandaa taarifa za utekelezaji wa mradi hususani taarifa za
masuala ya mazingira na jamii.
Kwa upande wake Mtaalamu Mkuu wa masuala ya Maendeleo ya Jamii
kutoka Benki ya Dunia Bw. Nicholas Soikan amesema kikao kazi hicho kina umuhimu
mkubwa kwa Uchumi wa mtu binafsi, familia, jamii na taifa kwa ujumla ili
kufikia malengo ya mradi huo.
Bw. Soikan ameongeza kuwa Benki ya Dunia kwa kushirikiana na
Serikali ya Tanzania wanatambua umuhimu wa asasi za kiraia na zina nafasi ya
kutatua migogoro ya ardhi inayojitokeza wanapoishi ili kutekeleza mradi kwa
ufanisi.
Kwa upande wao washiriki wa kikao kazi hicho kutoka asasi za
kiraia Bw. Jesta Twimanye kutoka Kahama na Bi Mwajumbe kutoka Mbinga wamesema
kuwa wamesema wanaendelea kushirikiana na Serikali katika mradi huo na
wanaendelea kutoa elimu juu ya haki ya umiliki wa ardhi kwa wanawake na wanaume
na mradi umesaidia kuongeza usalama wa ardhi kwa kutoa hati ya umiliki wa ardhi
kwa mume na mke.
Kikao kazi hicho kimehudhuriwa na wahamasishaji kutoka asasi za
kiraia kutoka Chalinze, Shinyanga, Kahama, Nzega, Kigoma, Mufindi, Mbinga,
Songwe, Tanganyika, Maswa, Chamwino, Kaliua, Uyuwi, Nkasi, Chunya, Ludewa,
Mkakete, Mvomero, Kilwa, Ruangwa, Kilindi, Mkinga, Handeni, Ngara, Rorya,
Iramba na Songea.
Comments
Post a Comment