WAZAZI NI KIUNGO MUHIMU UFAULU WA WANAFUNZI KISASA SEC
Na. Dennis Gondwe, DODOMA
WAZAZI wa wanafunzi katika Shule ya Sekondari Kisasa
wametakiwa kuwa kiungo muhimu baina ya walimu na wanafunzi katika malezi bora
na kuwasaidia wanafunzi kufaulu.
![]() |
Mjumbe wa Bodi ya Shule ya Sekondari Kisasa, John Komba akiongea na Jumuiya ya Shule ya Kisasa Sekondari |
Kauli hiyo ilitolewa na Mjumbe wa Bodi ya Shule ya
Sekondari Kisasa, John Komba kwa niaba ya Mwenyekiti wa Bodi ya shule hiyo
katika mahafali ya shule hiyo yaliyofanyika shuleni hapo.
Komba alisema “niwashukuru ninyi wazazi kwa kufika
kwenu na kutoa ushirikiano kwa wanafunzi wetu kwa ajili ya kuwapatia elimu.
Ninyi ni sehemu na msaada mkubwa kwa ajili ya kuwawezesha walimu waweze
kutimiza majukumu yao ya kuwalea na kuwafundisha wanafunzi wanapokuwa shuleni.
Na kwa wale wanaoshindwa kutimiza majukumu yao kama wazazi ndio usumbufu ambao
walimu wanaupata kutokana na ushirikiano mdogo kati ya wazazi na walimu na
kupelekea matokeo yasiyo mazuri kwa wanafunzi kuanzia malezi hadi taaluma.
Niwaombe wazazi tuendelee kutoa ushirikiano kwa walimu kwa ajili ya kumsaidia
mwanafunzi kupata elimu bora na malezi bora”.
Aliwataka wanafunzi wanapokuwa shuleni kufuata sheria
na taratibu zilizowekwa. “Sisi kama Bodi ya shule tutaendelea kufuata taratibu
zilizowekwa na tutaendelea kuwa wakali kwa wale watakaokiuka sheria na taratibu
za shule” alisema Komba.
Akiongea na wahitimu watarajiwa wa kidato cha Nne,
aliwapongeza kwa uvumilivu na kusoma kwa bidii kwa miaka minne. “Niwapongeze
sana tangu mmeanza kidato cha kwanza hadi kufika leo wanafunzi 233, ni kweli
baadhi yenu walishindwa kufikia hatua hii. Niwaombe sana wanafunzi wetu
mnaoenda kuhitimu na wale wanaoendelea na masomo kufuata sheria, kanuni na
taratibu za shule. Hatutamuonea aibu mtu, hatutarudisha nyuma msimamo wetu wa
kisheria, tutaendelea kuchukua hatua kali kwa wale wote watakaokwenda kinyume
na utaratibu wa shule” alisisitiza komba.
Aidha, aliwaombea heri katika mitihani yao inayofuata.
“Niwapongeze na niwatakie kila la keri katika siku zijazo za mitihani yenu.
Mwenyezi Mungu awatangulie awabariki sana asiwepo mtu wa kuugua mpaka ndoto
zenu zitakapokuwa zimetimia. Ninaona nyuso za madaktari hapa, wauguzi,
wahandisi na walimu hapa” aliongeza Komba.
Akiwasilisha taarifa ya Shule ya Sekondari Kisasa,
Mkuu wa shule hiyo, Mwl. Fredy Nyandoro alisema kuwa wahitimu hao walianza
masomo mwaka 2020. “Kwa heshima naomba kuwahudhurisha kwako wanafunzi 233 ambao
ni watahiniwa kwa mwaka huu 2023. Ndugu mgeni rasimi, shule yetu tumekuwa na
mafanikio kadhaa tangu kuanzishwa. Mafanikio hayo ni kuongeza ufaulu mwaka hadi
mwaka, kuongeza idadi ya watahiniwa na idadi ya vijana wanaojiunga elimu ya juu
na vyuo vya kati imeongezeka” alisema Mwl. Nyandoro.
![]() |
Mkuu wa shule ya Sekondari Kisasa, Mwl. Fredy Nyandoro akiongea na Jumuiya ya Shule ya Kisasa Sekondari |
Maeneo mengine aliyoyataja ni kuongeza miundombinu
mwaka 2019 walianza kujenga jengo la utawala ambalo limekamilika. “Mwaka 2021
tukapata mradi wa kuongeza madarasa kwa fedha za Uviko- 19 tulikuwa na madarasa
matatu na kufanya madarasa kufikia 23. Tunaishukuru sana serikali yetu na mama
yetu, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa uwekezaji mkubwa ambao ameufanya katika
sekta ya elimu na Shule ya Sekondari Kisasa ni mnufaika mkubwa wa uwekezaji
huo” alisema Mwl. Nyandoro.
Mwanafunzi wa kidato cha Nne, Nasra Waziri alifurahia
kuwa mwanafunzi wa shule hiyo. “Mimi nafurahia kuwa mwanafunzi wa Shule ya
Sekondari Kisasa inaonekana kuwa na sheria na taratibu zinazowalea wanafunzi
vizuri. Mimi tangu mwaka 2020 hadi sasa 2023 nimejifunza mambo mengi shuleni
hapa. Mimi nimeweza kuwa kiongozi na kujifunza “confidence” niliyojenga kuanzia
chini, hata hawa wabunge walianzia chini” alisema Waziri.
Akiongelea maandalizi yake kwa mtihani wa taifa wa
kidato cha Nne, alisema kuwa amejiandaa vizuri na kupata ufaulu wa kiwango cha
juu. “Tumeweza kujenga taswira nzuri katika shule yetu. Nimeweza kufurahia
mazingira ya shule yetu na jinsi walimu wanavyotoa ushirikiano kwetu” aliongeza
Waziri.
Ikumbukwe kuwa Shule ya Sekondari Kisasa ilianza mwaka
2006 ikiwa na wanafunzi 20 na walimu watatu sasa ina wanafunzi 869 na walimu
55.
MWISHO
Comments
Post a Comment