MBUNGE MAVUNDE AKABIDHI VIFAA VYA MAABARA VYA SH. 9,000,000/=
Na. Dennis Gondwe, KIKUYU KUSINI
ELIMU
ndiyo mkombozi kwa vijana wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma kwa lengo la
kuwasaidia kutoa mchango katika maisha yao na maendeleo ya taifa la Tanzania.
![]() |
Mbunge wa Jimbo la Dodoma Mjini, Anthony Mavunde akiongea na mamia ya walimu, wanafunzi na wananchi waliojitokeza katika hafla ya kugawa vifaa vya Maabara |
Kauli
hiyo ilitolewa na Mbunge wa Jimbo la Dodoma mjini, Anthony Mavunde alipokuwa
akiongea na wanafunzi na walimu wa shule za sekondari katika hafla ya kugawa
vifaa vya maabara kwa ajili ya masomo ya sayansi tukio lililofanyika Shule ya Sekondari
Wella iliyopo Kata ya Kikuyu Kusini.
Mavunde
ambae pia ni Waziri wa Madini alisema “elimu ninaamini kwamba ndiyo mkombozi wa
kweli kwa vijana wetu na elimu hii itawasaidia kwenda kuwafanya wakatoe mchango
wao na kulitumikia taifa la Tanzania na wao pia katika maisha yao. Baada ya
kubaini tunachangamoto katika maabara zetu nyingi za vifaa, nikasema nianze na
awamu ya kwanza na hii haitakuwa mwisho nitajitahidi kuzifikia maabara nyingi
zaidi. Leo nimeanza na shule tatu na mzigo wa kwanza huu umenigharimu shilingi 9,000,000
na nitaendelea kufanya hivi sababu dhamira yangu ni kuhakikisha wanafunzi wetu
wanafanya vizuri”.
Akielezea
mikakati yake kwa Halmashauri ya Jiji la Dodoma alisema ni kukuza elimu.
“Mkakati wa kwanza ambao ninao kwenye kukuza elimu katika Mkoa wa Dodoma na
hasa Jimbo la Dodoma mjini. Nimesikia changamoto ya walimu wa sayansi hii ni
changamoto kubwa na mimi suluisho ninalo na nimeshaanza kulifanyia kazi. Tuna
shule za sekondari 43, lakini Dodoma umepita Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano
ambao una uwezo wa kutuunganisha kupitia teknolojia ya kisasa mwalimu mmoja wa
sayansi mfano wa Shule ya Sekondari Msalato anaweza akawafundisha wanafunzi
wote wa Dodoma kwa wakati huohuo. Tukipata seti 43 za televisheni zikafungwa
shule zote, mimi kwa nafasi yangu nitakwenda kuongea na TCRA na watu wa Mfuko
wa Mawasiliano na kampuni za simu niwaombe watuunganishie huu mkongo” alisema
Mavunde.
Mkurugenzi
wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma, John Kayombo alisema kuwa halmashauri yake
imepeleka shilingi 20,000,000 kukamilisha ujenzi wa maabara ya shule ya Sekondari
Wella. “Mheshimiwa mbunge, hapa tayari unaona ujenzi unaendelea kwenye maabara
yetu kwa maelekezo ya Mheshimiwa Rais, sisi hatuwezi kukuangusha kwa sababu
tunafanya kazi kwa kushirikiana tumeshaleta shilingi 20,000,000 hapa kwa ajili
ya kukamilisha ujenzi wa maabara. Mheshimiwa waziri kwa maelekezo yako ya juzi
ulituelekeza tutafute fedha na tumeshapata shilingi 8,000,000 kwa ajili ya
kukamilisha matundu saba ya vyoo. Miongoni mwa changamoto ambazo zimezungumzwa
na mkuu wa shule nimezipokea na nitakaa na timu yangu ya menejimenti na
madiwani tuone namna bora ya kuzitatua” alisema Kayombo.
![]() |
Mkurugenzi wa Jiji, John Kayombo akisisitiza jambo |
Aidha,
alishukuru kwa vifaa vya maabara vilivyokabidhiwa na mbunge. “Mheshimiwa
waziri, vifaa hivi ulivyotukabidhi leo ninakushukuru sana, ni miongoni mwa
wabunge wachache wanaoyapenda majimbo yao. Mimi hii ni halmashauri yangu ya nne
kama mkurugenzi, lakini nimekuwa nikikufuatilia sana kote nilipokuwa unapambana
sana kuhakikisha jimbo lako linaenda vizuri, siyo kwenye elimu tu bali kwenye
maeneo yote. Nikuombe moyo huu uendelee na sisi tupo bega kwa bega na wewe
tutakupa ushirikiano wa kutosha na hakuna atakayekuangusha” alisema Kayombo.
Awali
akiongelea mafanikio ya shule hiyo Mkuu wa Shule ya Sekondari Wella, Mwl.
Adelifi Kaizirege alisema kuwa shule yake imefanikiwa kuongeza ufaulu wa
wanafunzi mwaka hadi mwaka. “Sambamba na hilo shule imefanikiwa kuongeza idadi
ya wanafunzi wanaojiunga kidato cha tano na vyuo vya kati. Kufanya ukarabati wa
vyumba vitatu vya madarasa kwa kuweka sakafu chini kupitia michango ya wazazi
na wadau wa shule na kuongeza vyumba vitatu vya madarasa” alisema Kaizirege.
Kuhusu
malezi na nidhamu ya wanafunzi alisema kuwa imeimarika sana. “Nidhamu ya
wanafunzi imeimarika kutokana na juhudi ambazo uongozi wa shule kwa
kushirikiana na walimu unazitumia na kuzisimamia. Wanafunzi wengi wanajitahidi
kuwahi kufika shuleni kutokana na usimamizi wa walimu. Uongozi wa shule
unawapongeza wazazi wote wanaotoa ushirikiano chanya katika kutatua changamoto
za kinidhamu zinazowakabili watoto wao hasa utoro, kunyoa mitindo, kutoboa pua,
kuvaa sketi fupi, kuvaa suruali zinazobana, kujihusisha kwenye mahusiano ya
kimapenzi na ugomvi” alisema Kaizirege.
Jumla
ya shule tatu za sekondari Wella, Makutopora na Mtemi Chiloloma zilipokea vifaa
vya maabara za masomo ya sanyansi vyenye thamani ya shilingi 9,000,000.
MWISHO
Comments
Post a Comment