JIJI LA DODOMA LAPELEKA MIL. 20,000,000 KUMALIZIA MAABARA

Na. Dennis Gondwe, KIKUYU KUSINI

HALMASHAURI ya Jiji la Dodoma imepeleka shilingi 20,000,000 kwa ajili ya ukamilishaji wa jengo la maabara katika Shule ya Sekondari Wella iliyopo Kata ya Kikuyu Kusini.

Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma, John Kayombo


Kauli hiyo ilitolewa na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma, John Kayombo katika hafla fupi ya kupokea vifaa vya maabara vilivyotolewa na Mbunge wa Jimbo la Dodoma mjini.

Kayombo alisema “Mheshimiwa mbunge hapa tayari unaona ujenzi unaendelea kwenye maabara yetu kwa maelekezo ya Mheshimiwa Rais, na sisi hatuwezi kukuangusha kwa sababu tunafanya kazi kwa kushirikiana. Tumeshaleta shilingi 20,000,000 hapa kwa ajili ya kukamilisha ujenzi wa maabara na inaenda kumaliziwa. Tunataka wanafunzi wetu waweze kufanya majaribio ya sayansi kwa vitendo. Mheshimiwa mbunge kwa maelekezo yako ya juzi ulituelekeza tutafute fedha na tumeshapata shilingi 8,000,000 kwa ajili ya kukamilisha matundu saba ya vyoo. Miongoni mwa changamoto ambazo zimezungumwa na mkuu wa shule nimezipokea na nitakaa na timu yangu ya menejimenti na madiwani tuone namna bora ya kuzitatua”.

Alishukuru kwa vifaa vya maabara alivyokabidhi Mbunge wa Jimbo la Dodoma mjini. “Vifaa hivi ulivyotukabidhi nikushukuru sana. Wewe ni miongoni mwa wabunge wachache wanaoyapenda majimbo yao. Nikuombe moyo huu uendelee na sisi tupo bega kwa bega na wewe tutakupa ushirikiano wakutosha na hakuna atakayekuangusha. Endelea kupiga kazi tupo pamoja na wewe usiku na mchana, muda wowote tutafutie vya kutosha huko” alisisitiza Kayombo.

Aidha, alimuombea kwa Mungu ili kukabiliana na changamoto za kazi. “Mheshimiwa mbunge nikuombe sana kwenye hizi kazi changamoto ni nyingi sisi tutaendelea kukuombea wala usikate tama, Mwenyezi Mungu atakubariki unafanya mengi mazuri hata Mungu anaona kwa hiyo, yale maneno ya kukukatisha tamaa achana nayo” alisema Kayombo.

Mbunge wa Jimbo la Dodoma mjini, Anthony Mavunde alikabidhi vifaa vya maabara za masomo ya sanyansi vyenye thamani ya shilingi 9,000,000 kwa shule tatu za sekondari Wella, Makutopora na Mtemi Chiloloma katika Jiji la Dodoma.




MWISHO

Comments

Popular Posts

Wananchi Makutupora wafunguka changamoto ya Maji, Umeme na Shule kwa Mkuu wa Mkoa

Waziri Mchengerwa apongeza usimamizi wa miradi jijini Dodoma

Mkataba ujenzi Uwanja wa Mpira wa Miguu wasainiwa Dodoma