MAANDALIZI UCHAGUZI MDOGO KATA YA NALA YAKAMILIKA
Na. Dennis Gondwe, Dodoma
WANANCHI wa Kata ya Nala wametakiwa kutumia haki yao ya
kidemokrasia kujitokeza kwa wingi kumchagua Diwani ili awawakilishe na kutetea
maslahi yao.
Kauli hiyo ilitolewa na Msimamizi wa Uchaguzi Jimbo la Dodoma
mjini, John Kayombo alipotembelea na kukagua vituo vya kupigia kura katika Kata
ya Nala.
Kayombo alisema “maandalizi ya uchaguzi mdogo wa Kata ya Nala
yamekamilika. Jumla ya vyama 11 vilichukua na kurejesha fomu na kupata nafasi
ya uteuzi wa kugombea nafasi ya udiwani wa Kata ya Nala. Kwa upande wa Tume ya Taifa
ya Uchaguzi ambayo mimi ndiyo Msimamizi wa Uchaguzi wa Jimbo la Dodoma mjini na
Kata ya Nala tumejiandaa vizuri na hatuna mapungufu yoyote”.
Alisema kuwa jumla ya wapiga kura wanaopaswa kupiga kura ni
3,741. “Niwaombe wananchi kujitokeza kwa
wingi ili kutumiza haki yao ya msingi kumchagua mwakilishi wao ambae ni Diwani
wa Kata ya Nala” alisema Kayombo.
Kata ya Nala inafanya uchaguzi mdogo kufuatilia kifo cha aliyekuwa
Diwani wa kata hiyo aliyefariki tarehe 10 Aprili, 2023 ikiwa na vituo 12 vya
kupigia kura.
Comments
Post a Comment