WAZAZI MTAA WA MAZENGO WASHAURIWA KULEA WATOTO KATIKA MAADILI
Na. Dennis Gondwe, CHANG’OMBE
WAZAZI wa Mtaa wa Mazengo Kata ya
Chang’ombe wametakiwa kijikita katika malezi ya watoto ili wawe na maadili mema
yatakayowawezesha kuwa raia wema na wawajibikaji katika jamii.
Afisa Ustawi wa Jamii wa Kata ya Chang’ombe, Debora Kanuya |
Kauli hiyoilitolewa na Afisa Ustawi
wa Jamii wa Kata ya Chang’ombe, Debora Kanuya alipokuwa akiongea na wananchi wa
Mtaa Mazengo kwenye mkutano wa hadhara ulioandaliwa na Chama Cha Mapinduzi (CCM)
na kufanyika katika Ofisi ya CCM Tawi la Chang’ombe Magharibi jijini Dodoma.
Kanuya alisema “ninawaomba sana akina
mama wa Mtaa wa Mazengo, tuwe na maneno mazuri kwa watoto wetu ili watoto
wanapokuwa wawe wanafahamu maneno mazuri, wasiwe na maneno ya matusi na maneno
ya mtaani. Lakini pia kuna baadhi ya akina mama ambao wamekuwa wakipiga sana
watoto wao na kutoa lugha ya matusi. Unakuta baadhi ya kina mama wametelekezwa
kwa hiyo zile hasira za kutelekezwa wanazihamishia kwa watoto, huo ni ukatili.
Niwaombe sana wanawake wenzangu tujikite katika malezi bora ya watoto wetu ili
waje kuwa viongozi na raia wema kama sisi. Sisi tusingepata malezi bora
tusingekuwa katika nafasi hizi na kuweza kuongea nanyi”.
Aidha, alikemea tabia ya baadhi ya
wanawake wanaokunywa pombe kupindukia. “Ndugu zangu kuna akina mama ambao
wanakunywa sana pombe. Kinachosikitisha zaidi wanakwenda na watoto vilabuni.
Kina mama wengine hawana muda na watoto wao, watoto wanashinda wakiwa wachafu,
wakiwa na njaa. Tuwatunze watoto wetu ili baadae pia watutunze” ailisema Kanuya
kwa uchungu.
Kwa upande wake Katibu wa Hamasa na Chipukizi
wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Dodoma, Nasra Seif alisema kuwa jamii
inatakiwa kuwalea watoto katika maadili mema ili kuwa na taifa imara lenye watu
wanaowajibika. “Siku hizi kumekuwa na tatizo kubwa sana la ukatili wa kijinsia
kwa watoto. Twende tukawalee watoto kwa maadili na nidhamu” alisema Seif.
Wananchi wa Mtaa wa Mazengo wakifuatilia mkutano wa hadhara |
Mkazi wa Chang’ombe, Juma Shaban
alisema kuwa changamoto kubwa kipindi hiki ni malezi ya watoto. Watoto
wanaanchiwa kujilea na kulelewa na makundi rika jambo linalosababisha kukuwa
bila maadili yaliyo mema kwa jamii.
MWISHO
Comments
Post a Comment