MALEZI YA WATOTO YANAMCHANGO KATIKA USALAMA KATA YA CHANG’OMBE
Na. Dennis Gondwe, DODOMA
AMANI na usalama wa Kata ya Chang’ombe
inatokana na jinsi jamii inavyowalea watoto katika misingi bora na maadili mema.
Kaimu Afisa Mtendaji wa Kata ya Chang’ombe, Daria Kapinga akiongea na wananchi |
Kauli hiyo ilitolewa na Kaimu Afisa
Mtendaji wa Kata ya Chang’ombe, Daria Kapinga alipokuwa akiongea na wananchi wa
Mtaa Mazengo kwenye mkutano wa hadhara ulioandaliwa na Chama Cha Mapinduzi na
kufanyika katika Ofisi ya CCM Tawi la Chang’ombe Magharibi.
Kapinga alisema “ninatamani
kuzungumza na mitaa miwili Mazengo pamoja na Msamalia suala la amani na ulinzi.
Mitaa yetu imekuwa ni mitaa ambayo inatajwa sana kwenye sifa mbalimbali. Lakini
chanzo nilichobaini ni kutoka kwenye mizizi ambapo ni kwa watoto wetu, kwenye
malezi ya watoto wetu tumeshindwa kuidumisha amani, tumeshindwa kudumisha
ulinzi kwa sababu ya malenzi tuliyonayo kwa watoto wetu. Malezi yasiyo mema kwa
watoto matokeo yake ya muda mrefu yanapelekea kwenye uvunjifu wa amani na
usalama”
Kapinga alisema kuwa imefika hatua mzazi analalamika kuwa mtoto wake ameshindikana na kusema hiyo ni hatua mbaya kimaadili.
“Hakuna mzazi anayetamani hata siku moja mtoto wake aharibikiwe, ila
siku hizi hayo mambo yamekuwa ni ya kawaida katika jamii zetu, imefikia hatua
mzazi anakwambia mtoto amemshindwa. Hakuna mtoto ambae atalelewa na ulimwengu,
kwenye suala la malezi usisubiri mtoto afike kwenye umri fulani anza nae sasa
akiwa mdogo. Hatutakuwa na Chang’ombe iliyo bora kama tusipokubali kubadilika
na kuwalea watoto wetu. Leo hii wengi wanalalamika wanafanyiwa vitendo vya
kikatili lakini tunaowaogopa ni watoto tuliowazaa wenyewe. Niwaombe sana
tubadilike katika kuwalea watoto wetu. Wazazi wetu wasingetulea vizuri hata
hawa viongozi wasingekuwepo” alisema Kapinga.
MWISHO
Comments
Post a Comment