WANANCHI MAZENGO WATAKIWA KULEA WATOTO KATIKA MAADILI

 Na. Dennis Gondwe, CHANG’OMBE

JAMII imetakiwa kuwalea watoto katika maadili mema ili kuwa na taifa imara lenye watu wawajibikaji.

Baadhi ya wananchi waliohudhuria mkutano wa hadhara


Kauli hiyo ilitolewa na Katibu wa Hamasa na Chipukizi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Dodoma, Nasra Seif alipokuwa akiongea na wananchi wa Mtaa Mazengo kwenye mkutano wa hadhara ulioandaliwa na CCM na kufanyika katika Ofisi ya CCM Tawi la Chang’ombe Magharibi.

Seif alisema “ndugu zangu tukiwalea watoto wetu katika maadili, tutakuwa na taifa ambalo ni imara lenye watu wanaowajibika ipasanyo. Siku hizi kumekuwa na tatizo kubwa sana la ukatili wa kijinsia kwa watoto. Twende tukawalee watoto kwa maadili na nidhamu. Kumbukeni alivyosema Afisa Mtendaji wetu wa Kata, Chang’ombe haitakuwa Chang’ombe ya matukio ya uhalifu, twende tukajifunze kutoka kwa wenzetu wa huko. Isionekane kama Chang’ombe ni sehemu ya watu ambao wameshindikana, hatutaki kuona ‘defender’ za Polisi zikipita Chang’ombe mara kwa mara kwa ajili ya uhalifu. Tumemsikia Afisa Ustawi wa Jamii wa Kata ya Chang’ombe alivyotoa elimu nzuri ya malezi ya watoto, tubadilike kuanzia sasa”.

Akiongelea umuhimu wa CCM kufanya ziara hizo, alisema kuwa ni utekelezaji wa maagizo ya Mwenyekiti wa CCM Taifa. “Ziara hii imefanyika si kwa bahati mbaya, Mwenyekiti wa CCM Taifa, Mama Samia Suluhu Hassan siku ya Mkutano Mkuu wa CCM Taifa alielekeza wanachama kwa ngazi zote waende kuhoji utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM. Watu wa Serikali kwa maana ya watendaji wa kata na mitaa, maafisa wote pamoja na wakuu wa divisheni waende wakawaeleze wananchi juu ya utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM ili tukirudi kwenye uchaguzi mkuu sisi kama Chama Cha Mapinduzi ambacho kinaomba ridhaa kwa wananchi tusiwe tuna maswali mengi ya kujibu kutoka kwa wapiga kura wetu” alisema Seif.

MWISHO

Comments

Popular Posts

Wananchi Makutupora wafunguka changamoto ya Maji, Umeme na Shule kwa Mkuu wa Mkoa

Waziri Mchengerwa apongeza usimamizi wa miradi jijini Dodoma

Mkataba ujenzi Uwanja wa Mpira wa Miguu wasainiwa Dodoma