Viwanda 17 vya kurejesha Taka za Plastiki vyaanzishwa Wilaya ya Dodoma

Na. Dennis Gondwe, DODOMA

WILAYA ya Dodoma imefanikiwa kuanzisha viwanda 17 vya kurejesha taka za plastiki na kugawa vifaa 12 vya kutenganisha na kuhifadhi taka kwa lengo la kuweka mazingira safi na salama kwa shughuli na maisha kuendelea.


Kauli hiyo ilitolewa na Katibu Tawala Wilaya ya Dodoma, Sakina Mbugi alipokuwa akisoma Risala ya Utii kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan wakati wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Wilaya ya Dodoma katika uwanja wa Shule ya Msingi Kizota jijini Dodoma.

Alisema kuwa wilaya kwa kushirikiana na wadau wa mazingira ilifanikiwa kuanzisha viwanda 17 vya kurejeresha taka za plastiki, kugawa vifaa 12 vya kutenganisha na kuhifadhi taka na elimu inaendelea kutolewa kwa wananchi, mashirika na taasisi katika kudumisha utamaduni wa usafi na uhifadhi wa mazingira. “Mheshimiwa Rais, wilaya inakadiriwa kuzalisha wastani wa tani 458 za taka ngumu kwa siku, ambapo wastani wa tani 305 sawa na asilimia 66.5 hupelekwa kwenye Dampo la kisasa Chidaya lenye ukubwa wa ekari 48“ alisema Mbugi.

Akiongelea eneo la Nishati safi, alisema kuwa wilaya inaendelea kuhakikisha wananchi wanahamia katika matumizi ya Nishati safi ya kupikia kwa kuhimiza utumiaji wa mkaa poa na gesi. “Aidha, tayari taasisi 379 za umma na binafsi zinazoandaa chakula cha watu wanaozidi 100 zimeacha matumizi ya mkaa na kuni ikiwa ni utekelezaji wa mikakati kufikia Dira ya Matumizi ya Nishati Safi 2030. Pia, zaidi ya mitungi 2,800 imegawiwa kwa mama na baba lishe, wanufaika wa mpango wa kunusuru kaya maskini na wajasiriamali kwenye kata“ alisema Mbugi.

Akiongelea sekta ya Maliasili, alisema kuwa kwa Mwaka 2025/2026, wilaya imefanikiwa kugawa, kuotesha na kustawisha miti 921,000 kwa kushirikiana na wadau mbalimbali na zoezi hili ni endelevu. Wilaya imetoa elimu na kutundika mizinga 16 ya nyuki na kuondoa makundi ya nyuki hatarishi kwa jamii, aliongeza.

MWISHO

 

Comments

Popular Posts

Wilaya ya Dodoma yapata “clean sheet” Miradi ya Mwenge wa Uhuru 2026