Mashine za Kieletroniki zakusanya Bil. 54.8 wilayani Dodoma

Na. Dennis Gondwe, DODOMA

WILAYA ya Dodoma imekusanya shilingi 54,886,235,688.85 sawa na asilimia 76.6 ya lengo la mwaka la kukusanya shilingi 71,675,239,000 kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026 kwa kutumia mashine za kieletroniki.



Kauli hiyo ilitolewa na Katibu Tawala Wilaya ya Dodoma, Sakina Mbugi alipokuwa akisoma Risala ya Utii kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan wakati wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Wilaya ya Dodoma katika uwanja wa Shule ya Msingi Kizota jijini Dodoma.

Akiongelea ukusanyaji kodi na mapato kwa mfumo wa TEHAMA, alisema kuwa wilaya inakusanya mapato ya serikali kupitia mfumo wa TAUSI. ”Mheshimiwa Rais, katika Mwaka wa Fedha 2023/2024 wilaya ilianza kutumia mfumo mpya uitwao TAUSI katika ukusanyaji wa vyanzo vyote vya mapato. Kwa kipindi cha kuanzia Julai, 2025 hadi Aprili, 2026, wilaya imefanikiwa kukusanya shilingi 54,886,235,688.85 sawa na asilimia 76.6 ya lengo la shilingi 71,675,239,000 kwa mwaka kwa kutumia mashine za kielektroniki” alisema Mbugi.

Kuhusu sekta ya biashara, alisema kuwa wilaya imefanikiwa kusajili wafanyabiashara kwenye mfumo wa serikali za mitaa kwa ukusanyaji mapato. ”Katika mwaka 2025/2026 wilaya imefanikiwa kutoa jumla ya leseni za biashara 17,521 ambazo zimeingiza shilingi 3,012,907,294 sawa na asilimia 76.6 ya lengo la mwaka na leseni za vileo 1,201 ambazo zimeingiza shilingi 63,955,000 sawa na asilimia 74.3 ya lengo la mwaka” alisema Mbugi.

Mwenge wa Uhuru Mwaka 2026 unaongozwa na kaulimbiu isemayo ‘Tanzania ni Yetu Sote, Tushikamane kwa pamoja Kuleta Maendeleo ’.

MWISHO

 

Comments

Popular Posts

Wilaya ya Dodoma yapata “clean sheet” Miradi ya Mwenge wa Uhuru 2026