Dodoma kuvuna Tani 40,930 Chakula na Nafaka

Na. Dennis Gondwe, DODOMA

WILAYA ya Dodoma inatarajia kuvuna tani 40,930 za mazao ya chakula na biashara katika kuwahakikishia wananchi lishe bora na kujikwamua kiuchumi.



Kauli hiyo ilitolewa na Katibu Tawala Wilaya ya Dodoma, Sakina Mbugi alipokuwa akisoma Risala ya Utii kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan wakati wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Wilaya ya Dodoma katika uwanja wa Shule ya Msingi Kizota jijini Dodoma.

Alisema kuwa wilaya kupitia Divisheni ya Kilimo Mjini na wadau iliendelea kuhakikisha wananchi wanapata lishe bora na kujikwamua kiuchumi kwa kulima mazao ya chakula na biashara. “Hali ya upatikanaji wa chakula na bei ni ya wastani kwa msimu wa kilimo 2025/2026. Wakulima wameanza kuvuna na kiasi cha tani 40,930 kinatarajiwa kuzalishwa. Hata hivyo, kuna mtiririko mzuri wa mazao ya chakula yanayoingia na kupatikana katika masoko yote. Hivyo, kuhakikisha upatikanaji wa chakula katika kipindi chote cha mwaka” alisema Mbugi.

Akiongelea sekta ya mifugo, alisema kuwa wilaya iliendelea kutoa huduma kwa wafugaji ikiwemo kutoa chanjo kwa mifugo, usimamizi na ukaguzi wa nyama ili kuhakikisha wananchi wanapata nyama safi na salama kwa ajili ya kulinda afya zao. Aliongeza kuwa wafugaji wanaendelea kupewa elimu ya kuboresha koosaafu za mifugo yao na usajili ili waweze kuongeza tija ya uzalishaji wa maziwa na kupunguza idadi ya mifugo na kukuwa kiuchumi. “Jumla ya ng’ombe 553 wamepandikizwa kwa chupa na ndama walioboreshwa 405 wamepatikana. Mheshimiwa Rais, wilaya imeweza kutoa elimu ya ufugaji wa samaki kwa wananchi ambapo hadi sasa kuna mabwawa 137 ya kufugia samaki yanayomilikiwa na wafugaji 95 na soko kubwa la samaki hao ni ndani ya wilaya. Pia leseni 243 zimetolewa kwa wafanyabiashara wa samaki ” alisema Mbugi.

Mwenge wa Uhuru Mwaka 2026 unaongozwa na kaulimbiu isemayo ‘Tanzania ni Yetu Sote, Tushikamane kwa pamoja Kuleta Maendeleo’.

MWISHO

 

Comments

Popular Posts

Wilaya ya Dodoma yapata “clean sheet” Miradi ya Mwenge wa Uhuru 2026