Ujenzi wa Barabara yenye urefu wa kilomita 1.6 fursa kwa wananchi wa Kata ya Nala

Na. Leah Mabalwe, NALA

Halmashauri ya Jiji la Dodoma ilitenga kiasi cha shilingi 2,431,050,561 kutoka mapato ya ndani kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 kwaajili ya mradi wa ujenzi wa barabara kutoka Hospitali ya Jiji mpaka barabara ya Singida yenye urefu wa kilomita 1.6 kwa kiwango cha lami.



Hayo yalibainishwa na Mhandisi wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Mhandisi Ally Bella alipokuwa akisoma taarifa ya ujenzi wa Barabara hiyo kwa Kamati ya Fedha na Utawala iliyofanya ziara ya kutembelea na kukagua miradi ya maendeleo kwa kipindi cha robo ya tatu ya mwaka wa fedha 2024/2025.

“Ujenzi huu wa barabara unajumuisha daraja kubwa la midomo mitatu pamoja na mingine minne ya duara. Pia utasaidia kwa kiasi kikubwa kwa wananchi ukizingatia katika barabara hii baadhi yao wanatoka sehemu mbalimbali kwaajili kufuata huduma za afya katika Hospitali ya Jiji na hii itarahisisha kutokana na miundombinu mizuri ya barabara na kuzifikia huduma za afya kirahisi” alisema Mhandisi Bella.


Pia alitoa shukrani kwa uongozi wa serikali ya awamu ya sita ikiongozwa na Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuleta maendeleo katika sekta mbalimbali ikiwemo barabara. “Sambamba na hayo nitoe shukrani zangu za dhati kwasababu serikali ya awamu ya sita ipo katika kukuza maendeleo. Kata ya Nala ni miongoni mwa kata ambayo imepiga hatua kubwa na hii ni kutokana na maendeleo yanayoletwa na Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan. Kulikuwa na changamoto ya hospitali lakini baada ya kutatuliwa changamoto hiyo pia serikali ikaamua kutuletea mradi wa barabara ambapo wananchi wananufaika nao” aliongezea Mhandisi Bella.

Utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa barabara ulianza tarehe 29 Novemba, 2024, baada ya mkataba kusainiwa tarehe 20 Novemba, 2024, na mkandarasi akiwa ‘Kings Builders Limited’ kwa gharama ya shilingi 2,431,050,561 kwa muda wa siku 270 na Msimamizi akiwa ni Mhandisi wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma.

MWISHO

Comments

Popular Posts

Osterbay Dodoma wajitokeza usafi wa mazingira

Usafi wa Mazingira Kipaumbele Kata ya Chamwino

Wananchi wa Kata ya Mtumba wanufaika na Mikopo ya asilimia 10 ya Halmashauri