Miundombinu chachu ongezeko uandikishaji wanafunzi Jiji la Dodoma
UBORESHAJI wa miundombinu ya elimu unaoendelea kufanywa na Serikali ya awamu ya sita chini ya Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan umekuwa chachu ya ongezeko la uandikishwaji wa wanafunzi wa darasa la kwanza na awali Jiji la Dodoma kutoka asilimia 98 hadi 115 kwa mwaka 2024.
Mkuu wa Divisheni ya Elimu ya Awali na Msingi Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Mwl. Prisca Myalla
Kauli
hiyo ilitolewa na Mkuu wa Divisheni ya Elimu ya Awali na Msingi Halmashauri ya
Jiji la Dodoma, Mwl. Prisca Myalla alipokuwa akiongelea mafanikio ya Serikali
ya awamu ya sita kwa miaka mitatu ofisini kwake.
“Divisheni
ya Elimu ya Awali na Msingi Jiji la Dodoma tunampongeza sana Rais, Dkt. Samia
Suluhu Hassan kwa kuendelea kuboresha miundombinu ya elimu na kutujengea shule
mpya kupitia mradi wa BOOST na EP4R. Halmashauri ya Jiji la Dodoma imeweza
kujengewa madarasa mapya na kuboreshewa miundombinu hali iliyopelekea wazazi na
jamii kuona fursa ya kuwaleta watoto wao kupata elimu. Serikali imejitahidi
sana kuhakikisha inasogeza huduma ya shule katika maeneo ya wananchi, sasa hivi
kwenye kata nyingi watoto wanapata elimu karibu na maeneo wanayoishi. Dhana
yakutomuandikisha mtoto shule kutokana na umbali imeisha na shule nyingi
zilizokuwepo zimeboreshwa. Hivyo, kutengeneza mazingira rafiki ya kujifunzia”
alisema Mwl. Myalla.
Akiongelea
mafanikio ya elimu katika kipindi cha miaka mitatu ya Serikali ya awamu ya sita,
alisema kuwa divisheni yake inajivunia ongezeko la ufaulu wa wanafunzi wa darasa
la saba kutoka asilimia 82.2 kwa mwaka 2021 hadi asilimia 93.18 kwa mwaka 2024.
“Ongezeko la miundombinu ya elimu limeenda sambamba na ufaulu wa wanafunzi
wanaohitimu darasa la saba. Halmashauri kwa sasa ufaulu umeongezeka hadi
kufikia asilimia 93.18. Hii ni kutokana na wanafunzi kusoma katika mazingira
mazuri na tulivu, ukilinganisha na miaka iliyopita. Pia serikali imeongeza
vifaa vya kufundishia. Sasa hivi kila mwalimu anatumia vifaa vya TEHAMA. Hivyo,
kuwafanya walimu na wanafunzi kwenda na mabadiliko ya sayansi na teknolojia”
alisema Mwl. Myalla.
Kwa
upande wake Mwalimu Mkuu Shule ya Msingi Dodoma English Medium, Mwl. Evodius
Kanizio aliishukuru serikali kwa kutoa fedha kiasi cha shilingi milioni 458
kwaajili ya ujenzi wa shule mpya ya mtaala wa kiingereza jijini Dodoma. “Shule
yetu ni shule ya mchepuo wa kiingereza inayomilikiwa na serikali, imeanza rasmi
mwaka 2024. Kwa sasa tuna jumla ya watoto 267 kuanzia darasa la awali hadi
darasa la tatu. Ujenzi wa shule hii umegharimu kiasi cha shilingi milioni 458
ambazo kati ya hizo milioni 400,000,000 zimetolewa na Serikali kuu na shilingi
milioni 58,000,000 zimetolewa na Halmashauri ya Jiji la Dodoma kupitia mapato
yake ya ndani. Tunamshukuru sana Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa nafasi hii
ya kutoa elimu bora kwa mtaala wa kiingereza kwa watazania. Hapo awali hatukuwa
na shule za mtaala wa kiingereza, tulizoea kujenga shule za mtaala wa kiswahili
ila kwa maono ya Rais wetu akaona tunaweza toa elimu bora ya kiingereza kama
shule nyingine za binafsi. Shule ambazo zitawafikia wananchi wa kipato cha kati
ambao hawawezi kumudu gharama za shule binafsi kupata elimu kwa gharama nafuu”
alisema Mwl. Kanizio.
Divisheni
ya Elimu ya Awali na Msingi Jiji la Dodoma inasimamia jumla ya shule 176 ambazo
kati ya hizo 104 ni za Serikali na 72 ni za watu binafsi, wanafunzi 138,679 na walimu
1862.
MWISHO
Comments
Post a Comment