KATA YA CHAMWINO YAADHIMISHA SIKU YA USAFI DUNIANI
Na. Dennis Gondwe, CHAMWINO
KATA ya Chamwino yaadhimisha maadhimisho ya Siku ya Usafi
Duniani kwa kufanya usafi wa mazingira katika maeneo mbalimbali ya kata hiyo.
Akiongelea maadhimisho hayo, Afisa Mtendaji wa Kata
ya Chamwino, Lucas Nkelege alisema kuwa maadhimisho hayo yamefanyika kwa
kufanya usafi wa mazingira katika barabara inayotoka makutano ya Wajenzi mpaka
kona ya Viva la vida. Alisema kuwa usafi huo ulihusisha kusafisha mtaro wenye
urefu wa mita 1,500.
“Usafi wa mazingira pia ulifanyika katika
mitaro yote inayozunguka Shule ya Sekondari ya Hijra na wananchi walijitokeza
na kufanya usafi katika korongo karibu na uwanja wa Shell Complex. Zaidi ya
kusafisha mitaro, usafi huo ulihusisha kutoa taka ngumu na kuokota makopo na
mifuko kwenye mtaro na maeneo ya pembezoni mwa barabara na korongo”
alisema Nkelege.
Akiongelea
mafanikio ya maadhimisho Siku ya Usafi Duniani, alisema kuwa yametokana na
ushirikiano wa karibu na wadau mbalimbali. “Napenda kutoa shukurani za dhati
kwa uongozi wa Kituo cha vipaji cha Shell Sports chini ya Mwenyekiti, Abdallah
Mohamed ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Kata ya Chamwino,
uongozi wa Shule ya Sekondari ya Hijra kwa namna wanavyozilea Club za Mazingira
tangu kuanzishwa kwake kwa kuwajengea vijana wadogo moyo wa kushiriki mambo ya
kijamii ikiwamo kudumisha usafi wa mazingira. Kwa uzito huohuo, shukrani ziende
kwa maafisa, Ally Mfinanga, Melania Mtui na Hadija Nyamsingwa kutoka
Halmashauri ya Jiji la Dodoma walioshirikiana nasi katika kufanikisha
maadhimisho haya” Nkelege.
Maadhimisho ya Siku ya Usafi Duniani mwaka 2023
yaliongozwa na kaulimbiu isemayo “Tuungane pamoja kujifunza, kupanga na
kuhimiza uimarishaji huduma za taka”.
MWISHO
Comments
Post a Comment