CHANG’OMBE WATAKIWA KUSAFISHA MAZINGIRA KUZUIA WAHALIFU
Na. Dennis Gondwe,
WAKAZI
wa Kata ya Chang’ombe wametakiwa kudumisha usafi wa mazingira kwa lengo la kuzuia
maficho ya wahalifu na kulinda afya zao ili waweze kufanya shughuli za
kujitelea maendeleo.
Kauli
hiyo ilitolewa na Afisa Mtendaji wa Kata ya Chang’ombe, Tunu Dachi alipoongoza
uzinduzi wa kampenzi ya usafi wa mazimgira katika kata hiyo tukio lililofanyika
katika Mtaa wa Mazengo jijini Dodoma.
Dachi
alisema “nilipofika Kata ya Chang’ombe niligundua kuwa kata yetu ni chafu sana.
Na katika kufanya vikao na wadau wa usafi wa mazingira tulikubaliana kuwa Mtaa
wa Mazengo ndio mtaa mchafu kuliko mitaa yote. Leo nataka tushirikishane jambo
rahisi sana, vikundi vya uzoaji taka vimeridhia kwamba kila Jumamosi wataungana
kwa umoja wao na jamii ya mtaa husika kuja kufanya usafi wa maeneo ambayo
mwenyekiti atakuwa amependekeza”.
Aliwataka
wananchi kujitokeza kwa wingi kushiriki katika mazoezi ya usafi wa mazingira
kila siku ya Jumamosi. “Kwa hiyo, mwananchi akisema anaenda kumfanyia mtu
usafi, hapana hatumfanyii mtu usafi tunajifanyia sote usafi. Jirani yako akiwa
msafi na wewe umesalimika, wewe ukiwa msafi na jirani yako amesalimika. Kutupa taka
ovyo ndio tunazalisha maficho ya vibaka na wavuta bangi. Sera yangu nataka Kata
ya Chang’ombe iwe safi na salama. Ulinzi na usalama unaanza kwenye usafi wa
mazingira” alisema Dachi.
Akiongelea
tabia ya baadhi ya wananchi kukaidi kujitokeza kushiriki mazoezi ya usafi wa pamoja
siku ya Jumamosi alisema kuwa wananchi wote wanatakiwa kujitokeza kushiriki
kufanya usafi. “Mwananchi kutoka kushiriki zoezi la usafi ni suala la lazima
siyo hiyari. Mwananchi atakayekiuka utekelezaji wa zoezi la usafi faini yake ni
shilingi 50,000. Leo tunapeana elimu Jumamosi ijayo tunatekeleza na
tutakayemkuta na makosa ya ziada faini inaenda mpaka shilingi 300,000.
Tujipende sisi na tuwapende jirani zetu. Mwananchi anayeelewa thamani ya afya
hawezi kugomea usafi, mkiwa wasafi maradhi yataondoka na kipato chenu
kitatumika kwa shughuli za maendeleo” alisema Dachi kwa msisitizo.
Alisema
kuwa zoezi hilo la usafi ni endelevu kwa mitaa yote ya kata hiyo. “Usafi siyo
suala la zimamoto, nataka Chang’ombe iwe safi. Halmashauri ya Jiji la Dodoma
inatoa vyeti, vifaa vya usafi kwa mtaa msafi na fedha zinatolewa hadi shilingi
8,000,000 za kutekeleza miradi ya maendeleo. Hivyo, kila mtu afanye usafi mita tano
kuzunguka nyumba yake” alisema Dachi akionesha matumaini ya mmoja ya mitaa yake
kuibuka mshindi wa usafi.
Kwa
upande wake, Jumanne Mwema alisema kuwa Chang’ombe inahitaji msisitizo mkubwa
katika usafi wa mazingira. “Alichosema huyu mama ni ukweli. Pita kwenye mitaa
utakuta uchafu umetakapaa, watoto wanacheza kwenye uchafu. Nimefurahi alipooanisha
usafi na afya za wananchi labda msisitizo ukiwekwa hapo watu wanaweza
kubadilika na kupenda kukaa na kufanya kazi kwenye mazingira safi” alisema
Mwema.
MWISHO
Comments
Post a Comment