Kata ya Ipala ipo mstari wa mbele katika Michezo
Na. Nancy Kivuyo, IPALA
Hamasa
ya serikali katika michezo nchini ni kichocheo cha wananchi wa Kata ya Ipala
kupenda kushiriki michezo ya aina mbalimbali kwa ajili ya kujenga na kuboresha
afya zao ili waweze kushiriki katika shughuli za maendeleo.
Diwani wa Kata ya Ipala, George Magawa |
Kauli hiyo ilitolewa na Diwani wa Kata ya Ipala, George Magawa alipokuwa akiongea na waandishi wa habari kuhusu nafasi ya michezo katika Kata ya Ipala walipotembelea kata hiyo.
Diwani
Magawa alisema kuwa serikali imekuwa inafanya hamasa kubwa katika michezo hali
iliyopelekea kata yao kuwa na mwamko mkubwa katika kushiriki mashindano
mbalimbali yanayoandaliwa katani hapo. “Kwakweli, mambo ya michezo tunaenda
nayo vizuri, kila mwaka tunafanya mashindano yanayoitwa ‘Magawa Cup’ ambayo
diwani ndiye mimi na kwa kushirikiana na mheshimiwa mbunge tuna ‘Mavunde Cup’,
tunaandaa mashindano hayo ili kuwasogeza wananchi karibu zaidi na michezo.
Wakati mwingine tunaunganisha michezo na kampeni za kijamii za serikali ili
kuwafikia wananchi wengi kwa mara moja. Yote hii ni katika kuiwezesha jamii
kujitambua na kuishi katika ile misingi ya utanzania. Kikubwa zaidi michezo
inasaidia kujenga na kuimarisha miili ya wanamichezo” alisema Magawa.
Akaongeza
kuwa wataendelea kuandaa mashindano na kuibua vipaji vya michezo ili kuchochea
wigo wa jamii kupenda michezo. “Michezo ni afya, tunamshukuru Rais wa Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania kwa kutuhamasisha kuboresha michezo katika maeneo yetu.
Ukiangalia fedha na zawadi anazotoa kwa timu zetu hapa nchini na makundi
mengine, inatia hamasa sana kwamba tukikazania jamii yetu huku chini kupenda
michezo itawasaidia huko mbeleni kufanya vizuri ndani na nje ya nchi. Tunaamini
wakati mwingine tutaboresha vipengele ili kuwavuta watu wengi kujumuika pamoja
na kuijenga Ipala imara kimichezo” alimalizia Magawa.
Nae Mtendaji
wa Kata ya Ipala, Herman Malindila alisema kuwa michezo inaunganisha jamii na
kupitia michezo wamekua wakitoa elimu mbalimbali kulingana na wakati kwa lengo
la kuijenga jamii iliyo bora katika kata hiyo. “Hapa katani michezo imekua
ikileta hamasa kubwa. Tumeendelea kuimaisha mahusiano mazuri miongoni mwetu na
hili tutaliendeleza chini ya mbunge wetu na diwani” alimaliza Malindila.
Kwa
upande mwingine, mkazi wa Kata ya Ipala, Amos Mdabuko, alimshukuru Mbunge Anthony
Mavunde na Diwani George Magawa kwa kuendeleza michezo katika kata yao na
kusema “nawashukuru sana viongozi wetu, wamekua mstari wa mbele kuhamasisha
jamii kushiriki na kupenda michezo. Jamii sasa hivi imeanza kuwa na mwamko wa
kupenda michezo, ndugu mwandishi, haya mashindano yakianza watu wanajaa sana
kushiriki, ninaamini mashindano ya awamu hii yatakua makubwa na ya kuvutia”.
MWISHO
Comments
Post a Comment