Wataalam wa Mawasiliano na Maendeleo ya Jamii washiriki kubainisha watoto wenye mahitaji maalum
Na. Aisha Ibrahim, DODOMA
Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la
Dodoma, Joseph Fungo, aliwataka watumishi wa Divisheni ya Elimu ya Awali na Msingi,
kuongeza wigo kwa kutumia wataalam wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini na Maendeleo
ya Jamii ili kuhakikisha wanasambaza taarifa za uhamasishaji na kubainisha
watoto wenye mahitaji maalumu katika jamii.
Fungo aliyasema hayo ofisini kwake alipopokea
taarifa ya ubainishaji wa watoto wenye mahitaji maalumu kwa mwaka 2025 kutoka Divisheni
ya Elimu ya Awali na Msingi Jiji la Dodoma baada ya kukamilika zoezi la utambuzi
na ubainishaji wa watoto wenye mahitaji maalum kwa jili ya kuandikishwa elimu
ya awali na darasa la kwanza zoezi lililoanza 07 hadi 22 Januari, 2025.
Akitoa pongezi kwa kazi nzuri ya ubainishaji
wa watoto wenye mahitaji maalumu, Kaimu Mkurugenzi, alisema kuwa serikali
inafanya juhudi kubwa kuhakikisha watoto hao wanapata haki stahiki na huduma za
msingi ili kujiona wako sawa na binadamu wengine. “Mpaka serikali inafanya
juhudi kubwa ya namna hii, maana yake kuna eneo ambalo watu wamejisahau na
kuwaweka watoto hawa pembeni, lakini ni watu ambao wanastahiri huduma kama zile
ambazo sisi tunapata” alisema Fungo.
Aidha, aliongeza kuwa Halmashaurii ya Jiji
la Dodoma, imejipanga kwa kutekeleza mradi mkubwa wa Kituo cha Mafunzo ya
Sayansi ili kuhakikisha kila mtoto anapata fursa ya kujifunza kwa vitendo mambo
mbalimbali kulingana na ewelewa wake binafsi. “Dodoma sasahivi tunafikiria
mambo makubwa na tuna mradi mmoja ambao tunatarajia kutekeleza Kituo cha
Mafunzo ya Sayansi. Kwahiyo, watoto watakao kuwa wanaingia pale watakuwa
wanaangaliwa, huyu ana uwelewa gani? Kama ni kompyuta basi apelekwe sehemu
husika na kama ana uwelewa wa magari basi apelekwe huko” alisema Fungo.
Kwa upande wake Afisa Elimu, Elimu Maalumu Halmashauri
ya Jiji la Dodoma, Mwl. Issa Kambi alichanganua kuwa katika ubainishaji wa
watoto wenye mahitaji maalumu, idadi yao jumla ni 218. Alisema watoto saba walipewa
rufaa ya kwenda hospitalini kutokana na changamoto maalumu za kiafya. Watoto 37
walipaswa kujiunga na shule maalumu, na kati ya hao, watoto 11 walitakiwa
kwenda shule jumuishi, na 39 walipangiwa kwenda vitengo maalumu lakini pia
watoto 11 walipangwa kwenda vyuo vya ufundi Singida kutokana na umri wao wa
kujiunga na elimu ya shule ya msingi kupita.
Sambamba na hayo, alisema katika zoezi hilo
walifanikiwa kwa kiasi kikubwa kupata watoto wengi katika kata mbalimbali ikiwa
ni kutekeleza agizo la Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma la uandikishaji
na ubainishaji wa watoto wenye mahitaji maalumu shuleni kwa ngazi ya awali na
msingi. “Tumefanikiwa kupata watoto wengi wenye mahitaji maalumu na wenye
kuhitaji hafua stahiki kama ambavyo tumeziwasilisha kwa Mkurugenzi wa Jiji la
Dodoma” alisema Mwl. Kambi.
Licha ya kuwepo mafanikio, Mwl. Kambi
alisema kuwa katika zoezi hilo wamekutana na changamoto mbalimbali ikiwemo
uhamasishaji duni ndani ya kata husika, idadi iliyozidi kwa watoto kuanzia
miaka 14, baadhi ya watendaji wa kata kutoa maelezo yasiyo jitosheleza, uwelewa
mdogo wa jamii kuhusiana na haki za watoto wenye uhitaji maalumu, mtazamo hasi
kwa watoto hao kuhusu suala la elimu na uwezo duni wa wazazi kuwapatia matibabu
stahiki watoto hao.
Pia, aliwashauri wazazi na walezi ambao bado
hawajapeleka watoto wao katika zoezi la ubainishaji, kuwapeleka watoto hao
katika shule zilizopo karibu yao ili wahusika wa zoezi hilo waweze kupata
taarifa kamili. “Ushauri wangu kwa wazazi ambao bado hawajawaleta watoto
kuwabainisha na pengine hawakupata taarifa vizuri wakati tunapita kwenye kata
hizo, wawapeleke kwenye shule zilizopo maeneo jirani ili kusudi wale walimu
waweze kutupatia taarifa mfumo wa ubainishaji ili tuweze kufika na kuwabaini
hao watoto” alisema Mwl. Kambi.
Lakini, aliiomba serikali kukamilisha na
kuboresha miundombinu ikiwa ni pamoja na kuongeza bweni lingine la Hombolo,
litakalo watengenezea mazingira rafiki watoto hao kupata elimu bora ili
kuendana na mahitaji yao. “Tunaomba tuweze kupata bajeti ya kuweza kujenga
bweni lingine jipya, kwasababu watoto hawa wanaongezeka kila kukicha” aliomba
Mwl. Kambi.
Serikali imekuwa mstari wa mbele katika
kufuatilia zoezi la uandikishaji na ubainishaji wa watoto wenye mahitaji
maalumu kuwa endelevu ili kuhakikisha watoto wanapata huduma zote za msingi na
haki stahiki kama binadamu wengine.
MWISHO
Comments
Post a Comment