Kata ya Mkonze yaanza mafunzo ya 10% kwa vikundi
Na. Dennis Gondwe,
KATA ya Mkonze imeanza kutoa mafunzo kuhusu mikopo ya
asilimia 10 inayotolewa bila riba na Halmashauri ya Jiji la Dodoma kwa vikundi
vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu kwa lengo la kuwajengea uelewa wa
uwepo wa mikopo hiyo na taratibu za kuipata.
Afisa Maendeleo ya Jamii Kata ya Mkonze, Theresia Camilius wakati akitoa mafunzo kwa vikundi vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu
Kauli hiyo ilitolewa na Afisa Maendeleo ya Jamii Kata
ya Mkonze, Theresia Camilius wakati akitoa mafunzo kwa vikundi vya wanawake,
vijana na watu wenye ulemavu katika Shule ya Msingi Mkonze iliyopo Kata ya
Mkonze Halmashauri ya Jiji la Dodoma.
Theresia alisema kuwa mafunzo hayo yanahusisha vikundi
vilivyosajiliwa na vinavyotarajia kuomba mkopo, vikundi ambavyo havijasajiliwa na
vinatarajia kuomba mkopo ili viweze kufahamu mchakato na kufanya usajili na
kuomba mikopo ya asilimia 10. “Matarajio ya mafunzo haya ni walengwa na
wanufaika wa mikopo hii waweze kuelewa fedha zinazotengwa kila robo ya mwaka na
Halmashauri ya Jiji la Dodoma ambazo ni asilimia 10 kwa ajili ya kuwezesha
vikundi vya wanawake asilimia nne, vijana asilimia nne na watu wenye ulemavu asilimia
mbili. Kwa kuwa mikopo hii ilisimamishwa kwa muda ili kufanya maboresho ya miongozo
na kanuni yaliyolenga kuwanufaisha watu wengi zaidi” alisema Theresia.
Alisema kuwa mafunzo hayo pamoja na mambo mengine
yanalenga kuwawezesha kuandika maandiko ya miradi na uandaaji wa katiba za
vikundi. Mafunzo yataendelea kwa kipindi cha wiki sita mfululizo yakihusisha
pia namna nzuri ya uendeshaji wa miradi na biashara, aliongeza.
Mafunzo hayo yalihusisha jumla ya vikundi 23, kati
yake, vikundi 13 vya wanawake, vikundi nane vya vijana na vikundi viwili vya
watu wenye ulemavu yakiwa ni mafunzo endelevu hata baada ya vikundi hivyo
kuhitimu mafunzo hayo yaliyogawanyika katika sehemu mbili ambazo ni mafunzo
kabla ya kuomba mkopo na mafunzo baada ya kuomba mkopo.
MWISHO
Comments
Post a Comment