KATA YA CHAMWINO YATAKIWA KUSIMAMIA UTEKELEZAJI MKATABA WA LISHE
Na. Dennis Gondwe, CHAMWINO
KATA ya Chamwino
imetakiwa kusimamia utekelezaji wa mkataba wa Lishe kwa mujibu wa maelekezo ya
serikali ili kukabiliana na tatizo la utapiamlo katika jamii.
Kauli hiyo ilitolewa
na Diwani wa Kata ya Chamwino, Jumanne Ngede aliyekuwa mgeni rasmi katika
maadhimisho ya Siku ya Afya na Lishe Mtaa wa Mailimbili aliyofanyika katika
mtaa wa Mailimbili.
Ngede alisema kuwa
ni jambo zuri kwa wataalam na Afisa Mtendaji wa Kata ya Chamwino kusimamia
suala la Lishe kutokana na umuhimu wake katika jamii. Alisema kuwa kutokana na
umuhimu wake, serikali ilisaini mkataba wa Lishe na makundi mbalimbali ili
watekeleze mkataba huo kwa kuhakikisha elimu ya Lishe inatolewa na utekelezaji
wa mkataba huo.
Kwa upande wake Afisa
Mtendaji Kata ya Chamwino, Lucas Nkelege alisema kuwa suala la utekelezaji wa
mkataba wa Lishe ni maelekezo ya serikali yanayotakiwa kutekelezwa kwa uzito
mkubwa. “Tumeshasaini mkataba wa Lishe, utakumbuka Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia
Suluhu Hassan alisaini mkataba na wakuu wa mikoa. Wakuu wa mikoa wakasaini na
wakuu wa wilaya. Wakuu wa wilaya wakasaini na wakurugenzi wa mamlaka za serikali
za mitaa, nao wakasaini wa maafisa watendaji wa kata. Maafisa watendaji wa kata
wakasaini na maafisa watendaji wa mitaa. Hii inaonesha umuhimu wa masuala ya Lishe
na afua zake katika jamii. Lengo kubwa ni kupunguza athari za utapiamlo katika
jamii” alisema Nkelege.
Alisema kuwa huduma
zilizotolewa katika maadhimisho hayo ni elimu ya Afya na Lishe, maonesho ya
makundi matano ya vyakula na upikaji wake, upimaji wa Afya ukihusisha kupima
HIV, uzito na urefu (BMI) pamoja na kutoa kutoa vyeti kwa watoto wadogo, matone
ya Vitamin "A" na kupima MUAC kwa watoto chini ya umri wa miaka mitano.
Afisa mtendaji huo
alisema matarajio ya utekelezaji wa mkataba wa Lishe, alisema kuwa ni kuona
hali ya lishe inabadilika na kuwa bora zaidi katika kata yake hasa kwa kina
mama wajawazito, watoto wenye umri chini ya miaka mitano na vijana balehe.
Akiongelea maadhimisho
hayo alisema kuwa ni utekelezaji wa kipengele namba mbili katika mkataba wa
lishe linachoelekeza kata na mitaa kufanya maadhimisho ya siku ya afya na lishe
ya mtaa (SALIKI) katika mitaa.
Maadhimisho ya siku
ya Afya na Lishe ya Mtaa hufanyika kwa mitaa yote kila baada ya miezi mitatu na
katika mtaa wa Mailimbili yaliongozwa na kaulimbiu isemayo “Lishe Bora kwa
Ustawi wa Afya zetu na Maendeleo ya Mtaa wetu” ukiwa ni mtaa wa pili
ukitanguliwa na mtaa wa Sokoine.
MWISHO
Comments
Post a Comment