DC SHEKIMWERI ASHAURI UTUNZAJI MAZINGIRA DODOMA
Na. Dennis Gondwe, KIKUYU KASKAZINI -DODOMA
WAKAZI wa Wilaya ya Dodoma wametakiwa kutunza na
kulinda Mazingira ili kujihakikishia uhai wa maisha ya wanadamu na viumbe hai.
Mkuu wa Wilaya ya Dodoma, Jabir Shekimweri akipanda mti katika Zahanati ya Kikuyu |
Kauli hiyo ilitolewa na Mkuu wa Wilaya ya Dodoma,
Jabir Shekimweri alipoongoza zoezi la usafi wa Mazingira na upandaji miti
kuzunguka Zahanati ya Kikuyu iliyopo Kata ya Kikuyu Kaskazini jijini hapa.
Shekimweri alisema kuwa uhai wa wanadamu upo kwenye
mazingira safi yenye miti mizuri. “Nisisitize mambo machache kwenye zoezi la
kupanda miti. Katika uumbaji Mwenyezi Mungu ametuumba kwa kutegemeane na
mazingira hakuna namna maisha yetu yatakuwepo pasina uwepo wa miti kwenye
mazingira yanayotuzunguka. Sisi tunatoa hewa inaitwa ‘carbon dioxide’ ambayo
kwa uumbaji wa Mungu hiyo ndiyo hewa safi kwa miti. Na yenyewe inatoa hewa
chafu ambayo inaitwa ‘oxygen’ ambayo kwa maisha ya wanadamu ndiyo hewa safi.
Kwa hiyo tunabadilishana hewa chafu kwa hewa safi” alisisitiza Shekimweri.
Alikemea tabia ya kukata miti. “Sote kwa pamoja
tukemee tabia ya kukata miti. Kwa maana hiyo ukiona mtu anakata mti kwa tafsiri
nyepesi anakuondolea hewa safi” alisema Shekimweri.
Aliwakumbusha maelekezo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania juu ya matumizi ya nishati mbadala. “Mhe Rais, Dkt. Samia Suluhu
Hassan aliekeleza kuanzia Januari mwakani matumizi ya mkaa yatakuwa marufuku.
Kila mmoja ajielekeze kwenye matumizi ya nishati mbadala. Kwa hiyo niwaombe
tujielekeze kwenye nishati mbadala kwa kufuata maelekezo mema ya Mheshimiwa
Rais. Kwa kufuata maelekezo hayo tulio wengi tutakuwa salama na dunia itakuwa
salama. Kwa watumishi wa umma natamani muwe wa mfano katika kuitikia maelekezo
ya serikali. Kunapokuwa hakuna wateja wa kununua mkaa maana yake hakutakuwa na
mzalishaji wa mkaa” alisema.
Mbunge wa Jimbo la Dodoma mjini, Anthony Mavunde akimwagilia maji mti aliopanda katika Zahanati ya Kikuyu |
Kwa upande wake Mbunge wa Jimbo la Dodoma mjini,
Anthony Mavunde aliwapongeza wakazi wa Kata ya Kikuyu Kaskazini kwa muitikio
wao katika kupanda miti na kufanya usafi kuzunguka Zahanati ya Kikuyu.
“Mheshimiwa Mkuu wa Wilaya ya Dodoma, nikushukuru sana kujumuika nasi siku ya
leo kufanya usafi katika Kata ya Kikuyu Kaskazini. Niwashukuru na wananchi kwa
kujitokeza kwa wingi kushiri mazoezi haya. Muitikio huu unaonesha kuwa
tunaelewa manufaa ya kupanda na kutunza miti katika mazingira yetu” alisema.
Aidha, aliupongeza uongozi wa Zahanati ya Kikuyu kwa
kuboresha mazingira ya zahanati hiyo. “Nitakuwa mnyimi wa fadhila
nisipomshukuru sana Mganga Mfawidhi wa Zahanati ya Kikuyu. Leo nimekuja
nimeshangaa sana mazingira ya hapa. Ametufundisha jambo kwamba lazima katika
maeneo yetu ya serikali tutunze na kuboresha mazingira. Zahanati ya Kikuyu
inapendeza na mimi nitawaunga mkono na kuipendezesha zaidi ili iwe kati ya
zahanati chache za mfano katika Jiji la Dodoma” alisema Mavunde.
Mwenyekiti wa Mtaa wa Serikali ya Mtaa wa Kikuyu,
Mohammed Mussa alisema “uongozi wa mtaa tunawahamasisha wananchi wote wa Kikuyu
washiriki mazoezi ya usafi na upandaji miti kwa sababu usafi unatupa afya na
kutufanya tuonekane wastaarabu na kudumisha mila za kitanzania. Uchafu ni tendo
baya linaleta magonjwa na kupunguza uwezo wa afya. Ukiwa huna afya huwezi
kufanya shughuli zako na taifa litaathirika kwa kuwa na watu wasio na afya
njema. Sambamba ya upandaji miti kwa lengo ya kutupatia hewa safi”.
Wadau wa Mazingira wakifuatilia hotuba ya Mkuu wa Wilaya ya Dodoma |
Jumla ya miti 30 ya matunda, kivuli na kupendezesha
madhari ilipandwa katika Zahanati ya Kikuyu katika halfa iliyoongozwa na Mkuu
wa Wilaya ya Dodoma na kuhudhuriwa na Mbunge wa Jimbo la Dodoma mjini,
Madiwani, maafisa waandamizi wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma, wanavyuo,
kikundi cha Kikuyu jogging na mamia ya wananchi wakereketwa wa uhifadhi wa
Mazingira.
MWISHO
Comments
Post a Comment