Wadau wa Lishe watakiwa kuzingatia Sheria
Na. Mwandishi wetu, DODOMA
Maafisa
lishe na watendaji wa kata wametakiwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu
katika utekelezaji wa shughuli za lishe pamoja na kuwashirikisha wadau
mbalimbali ili kuongeza ufanisi wa utekelezaji wa afua za lishe.
Kauli hiyo ilitolewa na Mwenyekiti wa Kikao cha Tathmini ya utekelezaji wa Mkataba wa Lishe kwa Robo ya Nne ya Mwaka wa Fedha 2025/2026, Sakina Mbugi alipoongoza kikao hicho kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya ya Dodoma kilichofanyika katika ukumbi wa mikutano wa halmashauri.
“Katika
utekelezaji wa shughuli za lishe ni muhimu kuwashirikisha wadau mbalimbali,
wakiwemo viongozi wa dini, wazee na vijana, ili kuwapatia uelewa kuhusu umuhimu
wa lishe bora. Tunapompa mzee elimu sahihi ya lishe, tunamsaidia kupunguza
changamoto za uzeeni na kujikinga dhidi ya magonjwa yasiyoambukiza. Hivyo,
nitumie nafasi hii kuwaelekeza maafisa lishe na maafisa watendaji wa kata
kuzingatia sheria, kanuni na taratibu katika utekelezaji majukumu yenu,”
alisema Mbugi.
Mwenyekiti
huyo ambae ni Katibu Tawala Wilaya ya Dodoma aliwapongeza maafisa watendaji wa
Kata za Mnadani, Kikuyu Kusini na Zuzu kwa kuendelea kuboresha utekelezaji wa
Siku ya Afya na Lishe (SALiKi). Vilevile, aliwasisitiza kuendelea kutumia
kaulimbiu ya lishe isemayo, “Zingatia Lishe Yako, Imarisha Afya, Akili na
Utendaji Kazi” ili kuhamasisha jamii kutambua umuhimu wa lishe bora.
Awali, akiwasilisha taarifa ya Tathmini ya utekelezaji wa Mkataba wa Lishe, Kaimu Afisa Lishe wa Jiji la Dodoma, Happiness Mlamka alisema kuwa shule zote zinaendelea kutoa chakula kwa wanafunzi, wajawazito wanapatiwa ‘Folic Acid’ kwa mujibu wa miongozo ya afya, shule zote zimeanzisha klabu za lishe kwa ajili ya kuwajengea wanafunzi uelewa kuhusu umuhimu wa lishe bora na akina mama wanaonyonyesha wanaendelea kuhamasishwa kuwanyonyesha watoto maziwa ya mama pekee katika kipindi cha miezi sita ya mwanzo wa maisha.
Aliongeza
kuwa kuanzia Julai, 2026 mfumo wa uwasilishaji wa taarifa za utekelezaji wa
shughuli za lishe utatumika mfumo wa kidijitali wa DHIS2, ukichukua nafasi ya
utaratibu wa awali wa kutumia makaratasi. Alieleza kuwa hatua hiyo itarahisisha
ukusanyaji, uwasilishaji na usimamizi wa taarifa za lishe na kuongeza ufanisi
katika utekelezaji wa afua za lishe.
Comments
Post a Comment