RC Senyamule apongeza ujenzi S/M Goba
Na. Mwandishi wetu, MKONZE
SHULE ya Msingi Goba iliyogharimu
shilingi milioni 302 imeongeza fursa ya upatikanaji wa elimu bora kwa watoto na
kuwapunguzia kutembea umbali mrefu kufuata shule katika maeneo mengine.
Kauli hiyo ilitolewa na Mkuu wa Mkoa wa
Dodoma, Rosemary Senyamule alipotembelea na kukagua mradi wa ujenzi wa Shule ya
Msingi Goba iliyopo Mtaa wa Muungano A, Kata ya Mkonze jijini Dodoma.
Mkuu wa mkoa aliipongeza Halmashauri ya
Jiji la Dodoma kwa kukamilisha mradi huo unaolenga kuongeza fursa za
upatikanaji wa elimu bora kwa watoto.
Vilevile, aliipongeza Halmashauri ya
Jiji la Dodoma kwa utekelezaji mzuri wa mradi huo na kusisitiza umuhimu wa
kuendelea kuwekeza katika miundombinu ya elimu ili kukidhi mahitaji
yanayotokana na ongezeko la idadi ya watu.
“Nawapongeza
kwa kukamilisha ujenzi wa shule hii kwa wakati na kwa viwango vinavyohitajika.
Hata hivyo, kutokana na kasi ya ukuaji wa Jiji la Dodoma, ni muhimu kuendelea
kujenga miundombinu zaidi ya elimu ili kuhakikisha kila mtoto anapata mazingira
bora ya kujifunzia," alisema Senyamule.
Alisema uwekezaji katika sekta ya elimu
ni msingi wa kuandaa kizazi chenye maarifa na ujuzi. Juhudi za serikali za
kuongeza shule na kuboresha mazingira ya kujifunzia zinapaswa kuendelea kupewa
kipaumbele, aliongeza.
Akizungumza kwa niaba ya wakazi wa Mtaa
wa Muungano A, Justine Mrema aliipongeza serikali kupitia Halmashauri ya Jiji
la Dodoma kwa ujenzi wa Shule ya Msingi Goba, akisema kuwa mradi huo umepunguza
adha iliyokuwa ikiwakabili watoto kutembea umbali mrefu kufuata masomo katika
Shule ya Msingi Mkonze.
“Kabla ya
shule hii kujengwa, watoto wetu walilazimika kutembea umbali mrefu kila siku
kwenda Shule ya Msingi Mkonze. Hali hiyo ilikuwa inawachosha na wakati mwingine
kuchelewa kufika shuleni. Sasa tunaishukuru serikali kwa kutusogezea huduma hii
muhimu, kwasababu watoto wetu watasoma katika mazingira salama na karibu na
makazi yao,” alisema Mrema.
Mradi wa ujenzi wa Shule ya Msingi Goba
ulianza tarehe 20 Novemba, 2025, umefikia asilimia 99 ya utekelezaji
ukijenga vyumba nane vya madarasa, yakiwemo madarasa sita ya elimu ya msingi na
mawili ya elimu ya awali, pamoja na jengo la utawala, matundu 10 ya vyoo kwa
elimu ya msingi na matundu sita ya vyoo kwa elimu ya awali chini ya ufadhili wa
Benki ya Dunia kupitia programu ya BOOST kwa gharama ya shilingi milioni 302.
Comments
Post a Comment