Jiji la Dodoma kinara utekelezaji afua za Lishe

Na. Mwandishi wetu, DODOMA

HALMASHAURI ya Jiji la Dodoma imepata alama ya kijani katika kadi alama ya viashiria vya utekelezaji wa afua za lishe ikiwa ni hatua nzuri kwa kipindi cha Robo ya Nne kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026.


Akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa shughuli za Lishe kwa kipindi hicho, Kaimu Afisa Lishe wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Happiness Mlamka alisema kuwa utekelezaji umeendelea kufanyika kwa mafanikio makubwa ambapo kadi alama ya lishe imeonesha rangi ya kijani. Alisema kuwa rangi hiyo ni kiashiria kwamba halmashauri imefikia viwango vinavyotakiwa katika utekelezaji wa afua za lishe.

Akizungumza katika kikao hicho, Mwenyekiti wake, Sakina Mbugi, aliyemuwakilisha Mkuu wa Wilaya ya Dodoma alipongeza Halmashauri ya Jiji la Dodoma kwa kuendelea kufanya vizuri katika utekelezaji wa shughuli za lishe. Alisisitiza umuhimu wa kuendeleza utoaji wa elimu ya lishe kwa kutumia kaulimbiu mbalimbali zinazotolewa kupitia Mbio za Mwenge wa Uhuru, ikiwemo “Zingatia lishe yako, imarisha afya, akili na utendaji kazi”.

Aidha, aliwataka maafisa lishe kuendelea kushirikisha makundi mbalimbali ya jamii, wakiwemo vijana, wazee, viongozi wa dini na viongozi wa kimila, katika utoaji wa elimu kuhusu umuhimu wa lishe bora ili kuongeza uelewa na kuimarisha afya za wananchi.



Mfumo wa tathimini, rangi ya kijani huonesha utekelezaji mzuri, rangi ya njano utekelezaji unaohitaji maboresho na ufuatiliaji zaidi na rangi nyekundu ikionesha kuna changamoto zinazohitaji hatua za haraka za kurekebisha.

 

Comments

Popular Posts

Jiji la Dodoma lashauriwa kulinda hadhi ya Makao Makuu ya Nchi

Afisa Biashara Arusha apongeza ukuwaji wa Biashara wa Jiji la Dodoma

Wakili Kipangula asisitiza weledi taaluma ya habari