Sekondari Zuzu yapongezwa usimamizi na utunzaji Mazingira

Na. Mwandishi wetu, ZUZU

SHULE ya Sekondari Zuzu imepongezwa kwa usimamizi mzuri wa shule na utunzaji wa mazingira jambo linalochochea utulivu wakati wa kufundisha na kujisomea kwa wanafunzi.


Kauli hiyo ilitolewa na Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Rosemary Senyamule alipotembelea na kukagua ujenzi wa mabweni mawili katika Shule ya Sekondari Zuzu.

Mkuu wa mkoa alimpongeza Mkuu wa Shule ya Sekondari Zuzu, kwa usimamizi mzuri wa shule hiyo. Alisema kuwa shule ina mazingira safi na rafiki kwa wanafunzi kujifunzia kwa utulivu na walimu kuweza kufundisha vizuri jambo lililopelekea shule hiyo kushika nafasi ya tisa kimkoa miongoni mwa shule za serikali.

Kwa upande wake Mkuu wa Shule ya Sekondari Zuzu, Mwl. Hezron Lupondo aliishukuru Halmashauri ya Jiji la Dodoma kwa kuendelea kuwekeza katika sekta ya elimu kupitia uboreshaji wa miundombinu ya shule.

“Ujenzi wa mabweni haya mawili umetupa hamasa kubwa sisi walimu na wanafunzi. Mazingira bora ya kujifunzia yanachangia kuongeza ari ya kufundisha na kujifunza. Hivyo, tunaamini yatachochea kufanya vizuri zaidi kitaaluma,” alisema Mwl. Lupondo.

Mbunge wa Jimbo la Dodoma Mjini, Pachal Chinyele alisema kuwa ameridhishwa na ubora wa mabweni yaliyojengwa katika shule ya sekondari Zuzu akiyataja kuwa yamejengwa kwa viwango vinavyokidhi mahitaji ya wanafunzi.

“Mabweni haya ni ya kisasa na yatasaidia kutatua changamoto zilizokuwa zinawakabili wanafunzi, hususan za malazi na usafiri. Haya ni mazingira yanayowapa nafasi nzuri zaidi ya kujifunza na kufanya vizuri kitaaluma,” alisema Chinyele.

Mradi wa ujenzi wa mabweni mawili katika Shule ya Sekondari Zuzu ulianza kutekelezwa tarehe 7 Aprili, 2025 ukiwa umefikia asilimia 99 ya utekelezaji wake umegharimu jumla ya shilingi milioni 331.

Comments

Popular Posts

Jiji la Dodoma lashauriwa kulinda hadhi ya Makao Makuu ya Nchi

Afisa Biashara Arusha apongeza ukuwaji wa Biashara wa Jiji la Dodoma

Wakili Kipangula asisitiza weledi taaluma ya habari