Mkurugenzi Mkuu wa TCAA Atembelea Maonesho ya Nanenane 2025 Jijini Dodoma
Na. Mwandishi wetu, DODOMA
Mkurugenzi
Mkuu wa Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA), Salim Msangi, atembelea
banda la TCAA pamoja na mabanda mengine kadhaa katika Maonesho ya Kilimo ya
Nanenane yanayoendelea katika viwanja vya Nzuguni jijini Dodoma. Ziara hii ililenga kuonyesha huduma zinazotolewa na TCAA na kuhamasisha umma
kuhusu masuala ya usafiri wa anga.
Katika ziara hiyo, Msangi alionesha kuridhishwa na namna TCAA inavyotoa huduma na elimu kwa wananchi, hasa kuhusu usalama wa anga, matumizi salama ya ndege zisizo na rubani (ndege nyuki), na fursa mbalimbali zilizopo katika sekta ya usafiri wa anga. Alieleza kuwa huduma zinazotolewa na TCAA zinachangia pakubwa katika kuimarisha usalama na maendeleo ya sekta hiyo.
Vilevile, alifurahishwa na ushirikiano wa watumishi wa TCAA katika kuelimisha
umma, akiwapongeza kwa kujituma na kuendelea kutoa taarifa muhimu kwa wananchi
kuhusu masuala ya usafiri wa anga. Alisisitiza umuhimu wa kuendelea
kushirikiana na wadau wengine katika kuleta maendeleo ya miundombinu ya
uchukuzi nchini.
Mbali na kutembelea banda la TCAA, Mkurugenzi Mkuu pia alikagua mabanda mengine
ya taasisi zilizo chini ya sekta ya uchukuzi, akisisitiza umuhimu wa mshikamano
na ushirikiano baina ya taasisi hizo. Aliweka wazi kuwa ni muhimu kwa taasisi
zote kufanya kazi kwa pamoja ili kukuza na kuimarisha huduma za uchukuzi na
usafiri wa anga.
Aliongeza kuwa TCAA itaendelea kushiriki kikamilifu katika matukio kama haya
ili kuimarisha utoaji wa elimu kwa umma na kuongeza uelewa kuhusu mchango wa
sekta ya usafiri wa anga katika maendeleo ya taifa.
Comments
Post a Comment