Mfumo wa Ufuatiliaji na Tathmini ni nyenzo ya utendaji kazi serikalini – Dkt. Biteko
Na. Mwandishi Wetu,
Naibu
Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Doto Biteko, amehitimisha Kongamano la
Nne la Kitaifa la Ufuatiliaji, Tathmini na Kujifunza lililofanyika jijini
Mwanza akiweka mkazo kuwa mfumo wa ufuatiliaji na tathmini ni nyenzo muhimu
katika kuhakikisha kuwa kila taasisi inatimiza wajibu wake kwa ufanisi na hivyo
kufikisha huduma bora kwa wananchi.
Kutokana
na hilo, Dkt. Biteko amewataka Wataalam wa Ufuatiliaji na Tathmini nchini
kufanya kazi kwa uaminifu na uadilifu bila kuogopa kuchukiwa kwani taifa
linawategemea ili kuweza kutoa huduma bora kwa wananchi.
“Hakuna
mtu au taasisi inayoweza kufanikisha majukumu yake bila kufanya tathmini, ninyi
ndio mnaoweza kutambua changamoto mapema na kuzitafutia suluhisho kabla
hazijawa kubwa, taasisi yoyote inayokosa mfumo huu inafanana na timu inayoingia
uwanjani bila refa..” alisema Dkt. Biteko.
Alitoa
mfano kuwa katika sekta ya umeme, kabla ya kupeleka huduma hiyo eneo lolote
lazima tathmni ifanyike ili kuepuka kurudia kazi mara mbili na pia tathmini
husaidia kuona matokeo ya huduma husika kwa wananchi.
Kuhusu
Kongamano hilo, Dkt. Biteko alieleza kuwa mwaka jana lilihudhuriwa na washiriki
900 huku mwaka huu likivutia washiriki 1,300.
Kwa
upande wake Mkuu wa Kitengo cha Ufuatiliaji na Tathmini (M&E) kutoka Wizara
ya Nishati, Anitha Ishengoma, alisema kuwa Wizara imejipanga kuimarisha mifumo
ya ufuatiliaji na tathimini ili kuboresha upatikanaji wa nishati ya uhakika na
nafuu kwa Watanzania.
Ishengoma alisema kuwa Sekta ya Nishati inahusisha taasisi kubwa sita pamoja na kampuni tanzu tano. Kila robo mwaka Wizara hufanya vikao vya kujadili tathmini ya utendaji kazi wa Wizara na Taasisi zake vinavyoongozwa na Waziri ili kujadili masuala mbalimbali kuhusu tathmini ya utendaji kazi ikiwemo kubainisha maeneo yenye changamoto zinazojitokeza na kuweka mikakati ya kuboresha utendaji kazi.
Kongamano
la Ufuatiliaji na Tathmini limewakutanisha wadau kutoka Taasisi za Umma na
Sekta Binafsi kwa lengo la kuimarisha mifumo ya ufuatiliaji na tathmini kwa
maendeleo endelevu.
Chanzo:
Michuzi Blog
Comments
Post a Comment