Prof. Mohamed ahimiza wanafunzi kusoma kwa bidii na kuwapongeza wazazi
Na. Mwandishi Wetu, DODOMA
Wanafunzi
wa Shule ya Sekondari Makutupora watakiwa kuwa na nidhamu na kusoma kwa bidii
ili kufikia malengo yao ya kielimu na maisha kwa ujumla.
Hayo aliyasema Katibu Mtendaji Baraza la Mitihani la Tanzania, Prof. Said Mohamed wakati wa Uzinduzi wa Upandaji Miti mwaka 2025/2026 uliofanyika katika Shule ya Sekondari Makutupora Jijini Dodoma.
Alisema
kuwa juhudi za wanafunzi katika masomo ni msingi muhimu wa maendeleo yao
binafsi na taifa kwa ujumla. “Msingi mzuri wa watoto ni kupata elimu hivyo
niwasihi wanafunzi muendelee kusoma kwa bidii ili kuweza kufikia ndoto zenu, kwasababu
hapa kuna viongozi wa baadae ambao wataweza kuongoza taifa letu, lakini pia muwe
na nidhamu kwasababu nidhamu ndio hupelekea kufika mbali hususan katika masomo
yenu” alisema Prof. Mohamed.
Aidha
aliwapongeza wazazi kwa juhudi wanazozifanya katika malezi ya watoto. “Nipende
kuwapongeza wazazi kwa namna ambavyo mnaendelea kuwalea watoto katika misingi
bora, lakini pia nisisitize ushirikiano kati ya wazazi pamoja na walimu
kwasababu ushirikiano ni nguzo muhimu katika kufanikisha elimu bora kwa watoto”
alisema Prof. Mohamed.
Kwa upande wake Mkuu wa Shule ya Sekondari Makutupora, Mwl. Didas Ndalu alimshukuru Katibu Mtendaji kwa kutembelea shule hiyo akieleza kuwa ujio wake ni faraja kubwa kwa wanafunzi na walimu. “Ni heshima kubwa kwetu kumpokea kiongozi huyu muhimu. Tunatarajia kuendelea kuinua kiwango cha taaluma na kuhakikisha wanafunzi wanapanda daraja mwaka hadi mwaka. Kutokana na walimu kuendelea kusimamia nidhamu ya wananfunzi ufaulu umeendelea kuongezea ikiwa kwa mwaka 2025 shule ilifaulu kwa GPA ya 3.4842, lakini pia tunaendela kuweka mikakati ya kuhakikisha tunafuta daraja sifuri na nne” alisema Mwl. Ndalu
Nae
mzazi alieshiriki katika uzinduzi wa upandaji miti, Phatina Mbeyu alisema
wazazi wataendelea kushirikiana na walimu katika kuhakikisha watoto wanalelewa
katika maadili mema. “Malezi bora kwa
mtoto yanachangia kwa kiasi kikubwa mafanikio katika masomo yao. Hivyo, ni
jukumu la kila mzazi kumsimamia mtoto katika malezi bora lakini pia ushirikiano
wa karibu baina ya mzazi na Mwalimu humjenga mtoto na tutaendelea kushirikiana
na walimu ili kuhakikisha wanafunzi wanazingatia elimu na kuwa na nidhamu”
alisema Mbeyu.
Uzinduzi huo wa upandaji miti ni juhudi za kuhifadhi mazingira sambamba na kuhamasisha jamii umuhimu wa utunzaji mazingira na kupanda miti.
MWISHO
Comments
Post a Comment