Mamia wajitokeza kuulaki Mwenge wa Uhuru 2026 Kata ya Kikuyu Kusini

Na. Dennis Gondwe, KIKUYU KUSINI

MAMIA ya wananchi wa Kata ya Kikuyu Kusini wamejitokeza wa wingi kuupokea Mwenge wa Uhuru ulipowasili katika Shule ya Sekondari Wella kuzindua mradi wa ujenzi wa vyumba viwili vya madarasa wenye thamani ya shilingi 42,800,000 fedha kutoka mapato ya ndani ya halmashauri.



Akiongelea wingi huo wa wananchi, Afisa Mtendaji Kata ya Kikuyu Kusini, Violet Oswald alisema kuwa muitikio wa wananchi kujitokeza kwa wingi utekelezaji wa misingi ya Mwenge wa Uhuru ya kuwaleta watu pamoja kwa upendo na kusisitiza umoja na mshikamano. “Wingi huu wa wananchi wa Kata ya Kikuyu Kusini ni utekelezaji wa kaulimbiu ya Mwenge wa Uhuru Mwaka 2026 isemayo ‘Tanzania ni yetu sote, tushikamane kwa pamoja kuleta maendeleo’. Hivyo, wananchi wamejitokeza kwa wingi kuupokea Mwenge wao na kushuhudia unavyozindua madarasa yao yaliyojengwa kwa fedha zao” alisema Oswald.

Akisoma taarifa ya mradi wa ujenzi wa vyumba viwili vya madarasa katika Shule ya Sekondari Wella kwa Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa Mwaka 2026, Kaimu Mkuu wa Shule, Mwl. Allen Lugemalila alisema kuwa madarasa hayo yamekuwa msaada kwa shule yake. “Ndugu Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa 2026, kupitia mradi huu, tumepata mafanikio yafuatayo katika shule hii. Mradi utapunguza msongamano wa wanafunzi madarasani na kuboresha mazingira ya kujifunzia na kufundishia. Hivyo, kuongeza kiwango cha ufaulu” alisema Mwl. Lugemalila.




Nae Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa, Wazo Mwang’onda alimpongeza Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuwekeza katika ujenzi wa miundombinu ya elimu. Kabla ya kuzindua mradi wa ujenzi wa vyumba viwili vya madarasa alikabidhi viti 40 na meza 40 vyenye thamani ya shilingi 5,460,000 fedha kutoka michango ya Mwenge wa Uhuru ya wananchi.

Mradi wa ujenzi wa vyumba viwili vya madarasa ulianza kutekelezwa tarehe 17 Novemba, 2025 na kukamilika tarehe 31 Januari, 2026 kwa kutumia mafundi wa ndani kwa gharama ya shilingi 42,800,000 fedha kutoka mapato ya ndani ya Halmashauri ya Jiji la Dodoma. Shule hiyo ina wanafunzi 915 na walimu 66.

MWISHO

 

Comments

Popular Posts

Baraza la Madiwani Jiji la Dodoma lawafukuza kazi watumishi watatu na mmoja kushushwa cheo