Wanawake TALGWU Dodoma wakabidhi Tenki la Maji lenye ujazo wa Lita 4,000
Na. Nancy Kivuyo, DODOMA
Kuelekea maadhimisho ya Siku ya
Wanawake Duniani, Kamati ya Ushauri Wafanyakazi Wanawake ya TALGWU Mkoa wa
Dodoma, imetembelea Kituo cha Afya Mkonze katika kufanya matendo ya huruma na
kukabidhi msaada wa tenki la maji lenye ujazo wa lita 4,000.
Akizungumza na uongozi wa Kituo cha
Afya Mkonze, Mwenyekiti wa Kamati ya Ushauri Wafanyakazi Wanawake ya TALGWU
Dodoma, Siwajibu Clavery alisema, “maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani yana
dhima kubwa sana hasa ukizingatia mwanamke ndio kinara wa majukumu kwenye
sehemu muhimu za familia. Sisi tumeona ni vema kufanya matendo ya huruma na
kutoa msaada wa tenki hili ili wagonjwa hasa wanawake waweze kupata huduma ya
maji wawapo katika matibabu kituoni hapa. Tunaomba mtumie kwa lengo hili
kusudiwa”.
Nae Mganga Mfawidhi wa Kituo cha Afya
Mkonze, Halima Kheri alisema anashukuru sana kwa msaada huo na atahakikisha
linatumika vema ili huduma ya maji ya ziada kituoni hapo isikosekane.
Msaada huo wa tenki la kuhifadhia maji
limegharimu kiasi cha shilingi 800,000 wakiwa na matajario ya kupunguza adha ya
maji katika Kituo cha Afya Mkonze.
MWISHO
Comments
Post a Comment