Kongamano kuhamasisha wanawake kugombea nafasi za uongozi lafanyika Dodoma
Na. Nancy Kivuyo, DODOMA
Kongamano la kanda ya kati likihusisha
mikoa ya Dodoma, Singida na Iringa lilifanyika katika ukumbi wa Jakaya Kikwete
huku kaulimbiu ikiwa ‘Wanawake na Wasichana 2025: Tuimarishe Haki, Usawa na
Uwezeshaji’.
Katika kongamano hilo, mada chokozi inayosema “Wanawake na Uongozi katika miaka 30 ya Beijing” iliandaliwa ambapo wanawake mashuhuri walialikwa kujadili mada na kutoa shuhuda mbalimbali za namna walivyoweza kufaulu katika harakati za kuwa viongozi na kushika nyadhifa mbambali nchini.
Akizungumza na maelfu ya wanawake
waliohudhuria katika kongamano hilo mgeni rasmi Spika Mstaafu wa Bunge la
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Anna Makinda alisema “wanawake changamkieni
fursa za uongozi kwasababu hata sisi tumekua mfano kwenu, angalieni mheshimiwa
rais wetu ni mwanamke anaiongoza nchi hii bila hofu, nyie mnashindwa hata
kugombea udiwani?. Akina mama amkeni, awamu hii tunaelekea kwenye uchaguzi
hivyo tunawategemea uwakilishi kwenye ubunge, udiwani na nafasi zingine”.
Nae Rhobi Maro aliyehudhuria kongamano
hilo alisema alifurahi kuhudhuria na kwamba alipata maarifa mengi na uthubutu
wa kufanya maamuzi. Aliongeza kuwa “naamini wanawake wengi watajitokeza
kugombea nafasi mbalimbali katika uchaguzi ujao sababu uwezo huo wanao na
natumai itakua hivyo”.
Kwa upande mwingine, Evelyn Alphonce alizungumza kuwa “siku ya leo imekua siku muhimu sana kuelekea kilele cha Siku ya Wanawake Duniani, nimefurahi kukutana na watu tofauti tofauti na kubadilishana nao mawazo, niseme tu nimehamasika”.
Kongamano hilo lilihudhuriwa na
wanawake wengi kutoka taasisi mbalimbali ikiwa ni shamrashamra za kujiandaa
kuelekea kilele cha madhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani kinachotarajiwa
kufanyika kitaifa Machi 8 mkoani Arusha ambapo mgeni rasmi atakua Rais wa Jamhuri
ya Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan.
MWISHO
Comments
Post a Comment