Wanawake watakiwa kujitathmini katika uongozi
Na. Faraja Mbise, DODOMA
Wanawake watakiwa kujitathmini katika nyanja
za uongozi kwa kuonesha nia ya kuwajibika ipasavyo na kuchangamkia fursa za
uongozi zinazojitokeza katika jamii.
Kauli hiyo ilitolewa na Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Rosemary Senyamule alipokuwa akizungumza na maelfu ya wanawake waliojitokeza katika kongamano la kanda ya kati lililohusisha mikoa mitatu (Dodoma, Singida na Iringa) katika kuelekea kilele cha Siku ya Wanawake Duniani kongamano hilo lilifanyika katika ukumbi wa Jakaya Kikwete Convention Centre, Dodoma.
Senyamule alisema “naomba nitoe shime kila
mmoja wetu ajitathmini hatua gani amechukua kuonesha uwezo wake wa kuongoza
katika eneo alilopewa. Ni imani yangu kuwa kila mahali tunatosha kwasababu Rais,
Dkt. Samia Suluhu Hassan ameonesha uwezo wa kutosha kwenye nafasi ya urais. Kwahiyo,
wanawake tunaweza katika kila eneo”.
Akiongelea kuhusu takwimu za wanawake
viongozi wa Mkoa wa Dodoma, alisema karibu ngazi zote za uongozi kuna viongozi
wa kike na takwimu zinaonesha uthubutu ni mdogo na hivyo aliwataka wanawake
kuongeza uthubutu wa kuwanania nafasi hizo za uongozi.
“Mkuu wa mkoa kwa sababu anatakiwa mmoja,
kwahiyo ni asilimia 100 inaongozwa na mwanamke, kwa wakuu wa wilaya ni asilimia
71, kati ya wakuu wa wilaya saba wawili ni wanaume na watano ni wanawake na
wanafanya vizuri katika nafasi zao. Tukienda upande wa wabunge, asilimia 11 ni wanawake,
katibu tawala tuna asilimia 86, wakurugenzi wa halmashauri asilimia 25 na madiwani
asilimia 14 za wanaogombea ni wanawake” alisema Senyamule.
Kwa upande wake, Mfamasia kutoka Hospitali ya Rufaa, Mkoa wa Dodoma, Jackline Moshi, alisema kuwa amejifunza mengi katika kongamano hilo na kuchangamkia fursa zinazojitokeza katika jamii.
“Tumejifunza mengi sisi kama wanawake,
tukayafanyie kazi hasa kujiamini katika nyanja mbalimbali za uongozi, kujiamini
katika kufanya kazi, kujiamini katika kila sekta. Tukisimama na wanaume
tunaweza” alisema Moshi.
Nae, mkazi wa Dodoma, Rhobi Maro alisema
amevutiwa sana na rai iliyotolewa na Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Rosemary Senyamule
na Spika mstaafu wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Anna Makinda ya
kuchangamkia fursa katika uongozi. Pia alitoa rai yake kwa wanawake kuendelea
kujiamini na kupambana kuchangamkia fursa zinazojitokeza.
“Wameongelea kuchangamkia fursa kujitokeza
hasa katika kugombea na kupambana zaidi. Na tunaamini wanawake wengi
watajitokeza katika uchaguzi huu wa 2025 kugombea nafasi mabalimbali za
uongozi. Natoa rai kwa wanawake wote waendelee kupambana na kujiamini kwamba
wanaweza” alisema Maro.
MWISHO
Comments
Post a Comment