Jiji la Dodoma latoa elimu dhidi ya ukatili wa kijinsia kwa wanafunzi wa kike
Na. Nancy Kivuyo, DODOMA
Ofisi ya Mkurugenzi wa Jiji la Dodoma
kupitia Divisheni ya Maendeleo ya Jamii, walitoa mafunzo kwa wanafunzi wa Shule
za Sekondari Viwandani na Kikuyu ikiwa ni shamrashamra za kueleka kilele cha
maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani itakayofanyika kitaifa mkoani Arusha
tarehe 08 Machi, 2025.
Akizungumza na wanafunzi wasichana
kwenye shule hizo, Afisa Maendeleo ya Jamii, Dawati la Msaada wa Kisheria,
Elizabeth Godwin alisema “tupo katika kuhakikisha binti anapata elimu kuhusiana
na masuala ya ukatili wa kijinsia kwasababu tunaamini ya kwamba, binti
anapofanyiwa ukatili wa kijinsia ndio tunapoteza ule uhalisia wa mwanamke ambae
baadae ndio angekuja kuwa nguzo muhimu ya familia kama mlezi au mzazi mzuri.
Tushukuru Mungu wanafunzi wameitikia wito wa elimu hii nzuri, wameonesha
kuelewa juu ya elimu ya ukatili na mahali gani pa kuripoti”.
Nae Mratibu wa Elimu Kata ya Viwandani,
Zaituni Mkoyi aliwaasa wasichana wanafunzi kuzingatia masomo ili waje kuwa
mfano mzuri katika maisha yao ya sasa na ya baadae. “Hata sisi tulikua watoto
kama ninyi, lakini tulisoma kwa bidii na kuchangamkia fursa mbalimbali ndio
maana mnatuona leo hapa. Hata nyie mnaweza, msome kwa bidii, muwe watoto
wasikivu, muwe na heshima kwa wazazi na wakubwa zenu na hakika mtafanikiwa”
alisema Mkoyi.
Kwa upande mwingine, Mwanafunzi
Conjesta Mwanika alisema kuwa amejifunza vitu vingi katika mafunzo hayo na
anaamini atasoma kwa bidii na kufuata ushauri makini uliotolewa. “Nimejifunza
vitu vingi sana leo, la kwanza tuzingatie masomo, tuwe na nidhamu, tuchangamkie
fursa za kujishughulisha na kilimo cha vitalu, kufanya biashara ndogo ndogo ili
kujikimu na kukwepa tamaa” alisema Mwanika.
Nae Mwanafunzi, Jenipha Mandela alishukuru
kwa mafunzo hayo na kuahidi kusoma kwa bidii ili kuweza kufikia ndoto zake. Aliongeza
kuwa amepata elimu kubwa juu ya masuala ya ukatili wa kijinsia na kusema
“ukatili wa kijinsia unaweza kutuathiri kisaikolojia, hivyo tunapaswa kuripoti
matendo mabaya kwa mwalimu wa Malezi au jirani ambae ni mshauri mzuri ili aweze
kutusaidia katika kutatua tatizo hilo” alisema Mandela.
MWISHO
Comments
Post a Comment