Wananchi Kata ya Chang’ombe wahimizwa kulinda miundombinu

Na. Mwandishi Wetu, DODOMA

Wananchi wa Kata ya Chang’ombe watakiwa kuendelea kuitunza na kuilinda miradi ya maendeleo ili iweze kutoa huduma kwa muda mrefu na kuvinufaisha vizazi vya sasa na vijavyo.



Hayo aliyasema Naibu Meya wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Bakari Fundikira mara baada ya kutembelea na kukagua utekelezaji wa miradi ya maendeleo katika Kata ya Chang’ombe jijini Dodoma.

Alisema kuwa serikali imeendelea kuwekeza fedha nyingi katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo yenye lengo la kuboresha huduma za kijamii na kuinua ustawi wa wananchi. “Hivyo, ni wajibu wa kila mwananchi kushiriki katika kuilinda na kuitunza. Leo tumetembelea miradi mbalimbali ikiwemo ujenzi wa Ofisi ya Mtaa wa Kishoka, Ofisi ya Mtaa wa Chang’ombe Juu, Ofisi ya Mtaa wa Hamvu, kisima cha maji Shule ya Msingi Chang’ombe na

ujenzi wa Wodi ya Mama na Mtoto katika Kituo cha Afya Chang’ombe ambapo miradi hii imejengwa kwa fedha za serikali jumla ya shilingi 456,926,355. Lakini pia nitoe rai kuwa ni muhimu kila mmoja wetu awe mlinzi wa maendeleo haya kwa kuitunza, kuilinda na kuhakikisha inatumika kwa malengo yaliyokusudiwa ili iendelee kuwanufaisha wananchi kwa miaka mingi ijayo,” alisema Fundikira.

Aliongeza kuwa ushirikiano kati ya wananchi na serikali ni msingi muhimu wa kuhakikisha uwekezaji unaofanywa unaendelea kuleta matokeo chanya katika sekta mtambuka.

Kwa upande wake Afisa Mtendaji wa Kata ya Chang’ombe, Hussein Kabezi alisema kuwa anaishukuru serikali kwa ujenzi wa miradi hiyo kwasababu imekuwa na mchango mkubwa kwa maendeleo ya wananchi.

“Miradi hii imekuwa na mchango mkubwa katika kuboresha upatikanaji wa huduma kwa wananchi na tunaahidi kuwa tutaendelea kushirikiana na wakazi wa kata hii na kuhakikisha miundombinu yote inalindwa dhidi ya uharibifu,” alisema Kabezi.

Comments

Popular Posts

Jiji la Dodoma lashauriwa kulinda hadhi ya Makao Makuu ya Nchi

Uwanja wa Maonesho wa Nanenane wafurika

TAMISEMI yakusanya Shilingi Trilioni 1.11