Ujenzi wa madarasa 3 S/M Mazengo kukamilika Julai, 2026

Na. Mwandishi wetu, KIKUYU KASKAZINI

 

Uongozi wa Mtaa wa Kigamboni, Kata ya Kikuyu Kaskazini umepongeza kasi ya ujenzi madarasa matatu katika Shule ya Msingi Mazengo kwa gharama ya shilingi 71,373,640 kwa lengo la kuboresha mazingira ya wanafunzi kujifunzia na kuelekeza mradi huo kukamilika kwa wakati.

 


Pongezi hizo zilitolewa na Afisa Mtendaji Kata ya Kigamboni, Farijala Kunga alipoongoza wajumbe wa Serikali ya Mtaa wa Kigamboni na maafisa ugani wa Kata ya Kikuyu Kaskazini kutembelea na kukagua maendeleo ya ujenzi wa madarasa matatu katika Shule ya Msingi Mazengo.

Alisema kuwa wameridhika na kasi ya ujenzi wa madarasa hayo ambayo yanatarajiwa kukamilika Mwezi Julai, 2026 kabla ya shule kufunguliwa. “Ni matumaini yangu kuwa ujenzi huu utakamilika kwa muda ulipangwa ili wanafunzi watakapofungua shule waweze kuyatumia. Madarasa haya ni utekelezaji wa ahadi ya Rais, kuleta tabasamu kwa wananchi, hapa ni wanafunzi na walimu watakaotabasamu” alisema Kunga.

 Aidha, aliishukuru Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA) kwa kufadhili ujenzi huo. “Ni tumie nafasi hii kuishukuru sana TEA, kuwa kutoa fedha shilingi 71,373,640 za ujenzi wa madarasa haya matatu. Mtaa wa Kigamboni tunaishukuru sana TEA kwa kuwa mdau mkubwa wa elimu, na kupitia ujenzi wa madarasa haya kupunguza upungufu wa madarasa na kuongeza kiwango cha ufaulu kwa wanafunzi” alisema Kunga.

 Kwa upande wake Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Mazengo, Mwl. Rehema Nkungu alisema kuwa atahakikisha ujenzi wa madarasa hayo unakamilika kwa wakati ili wanafunzi wanapofungua shule waanze kuyatumia. Aliongeza kuwa ujenzi huo ni juhudi za serikali ya awamu ya sita za kukabiliana na changamoto ya upungufu wa miungombinu ya elimu ikilenga kuboresha mazingira ya kufundishia na kujifunzia.

Mtaa wa Kigamboni unaendesha Kliniki ya siku tatu kuanzia tarehe 11-13 Juni, 2026 ya kutoa huduma kwa wananchi zikiwemo upimaji wa afya, msaada wa kisheria zikihusisha wadau wengine kama benki ya NMB, RITA, TRA na NSSF pamoja na kusikiliza na kutatua kero zao.

MWISHO

Comments

Popular Posts

Bodaboda Mtaa wa Kigamboni wanufaika na Kliniki ya kutatua kero