Mtakwimu Mdoya mbabe Mchezo wa Drafti

Na. Shahanazi Subeti, DODOMA

Mtakwimu wa Jiji la Dodoma, William Mdoya ameibuka mshindi katika Mchezo wa Drafti baada ya kumfunga Afisa Michezo, Peter Ititi kwa jumla ya mabao 2-1 ambapo mchezo huo ulilazimika kwenda kwenye muda wa ziada baada ya muda wa kawaida kufungana bao 1-1.




Baada ya ushindi huo alisema “nafurahia ushindi kwa sababu ndio kitu nilichokuwa nakitarajia katika bonanza hili, mchezo ulikuwa mzuri, wachezaji wote niliokutana nao walikuwa wazuri na walionesha ushindani ndiyo maana katika mchezo wa fainali tulienda hadi muda wa ziada” alisema Mdoya.

Nae, Mwalimu Stephen Sebastian, ambaye ni mmoja wa washiriki wa mchezo wa Drafti amekiri kushindwa, hii ni kutokana na ubora wa mpinzani wake. “Mpinzani wangu alikuwa ni mzuri na anaonekana ni mzoefu katika kucheza drafti na katika mchezo ninakiri kwamba, kuna kushindwa na kushinda na nakubali mpinzani wangu amenizidi mbinu na ujanja katika mchezo huu” alisema Sebastian.

Kwa upande wake Mwamuzi wa Mchezo wa Drafti, Evance Msilu, ametoa ufafanuzi wa mchezo na kuweza kumpata mshindi katika mashindano hayo. “Mchezo ulikuwa ni wa kishindani zaidi kwasababu fainali ilikuwa ni ya moto, kulikuwa na timu nane kwa kila idara lakini idara nyingine zilishindwa” alisema Msilu.

Mchezo huo umechezwa leo katika Uwanja wa Jamhuri Dodoma na ulihusisha wafanyakazi wote wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma katika CCD Watumishi Bonanza lililoandaliwa na Halmashauri ya Jiji la Dodoma kwa ajili ya kuukaribisha Mwaka 2025 likiongozwa na kaulimbiu isemayo ‘Halmashauri ya Jiji la Dodoma 2025 Ushirikiano na Umoja Wetu Ndiyo Nyenzo ya Huduma Bora.

MWISHO 

 

 

 

Comments

Popular Posts

Wananchi Makutupora wafunguka changamoto ya Maji, Umeme na Shule kwa Mkuu wa Mkoa

Waziri Mchengerwa apongeza usimamizi wa miradi jijini Dodoma

Mkataba ujenzi Uwanja wa Mpira wa Miguu wasainiwa Dodoma