Shilingi 698,800,161 zatekeleza mradi wa Nishati safi Sec Dr. Samia- Dodoma


Na. Dennis Gondwe, IYUMBU

SHILINGI 698,800,161 za utekelezaji wa mradi wa Nishati safi ya kupikia katika Shule ya Sekondari Dr. Samia-Dodoma zimelenga kuhifadhi Mazingira kwa kurejesha taka, kupunguza matumizi ya kuni na mkaa na kulinda afya za watumiaji.



Kauli hiyo ilitolewa na Mkuu wa Shule ya Sekondari Dr. Samia-Dodoma, Mwl. Leticia Singo alipokuwa akisoma taarifa ya mradi wa nishati safi ya kupikia kwa Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru kitaifa 2026 shuleni hapo.

“Ndugu Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa 2026, lengo la mradi ni kuhifadhi Mazingira kwa kurejesha taka zinazozalishwa shuleni pamoja na kupunguza madhara yatokanayo na matumizi ya kuni na mkaa kwa kutumia nishati safi ya kupikia” alisema Mwl. Singo.

Alisema kuwa mradi huo ulitekelezwa kwa gharama ya shilingi 698,800,161 fedha kutoka mradi wa P4R chini ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia chini ya Mkandarasi SUMA JKT. Akiongelea mafanikio ya mradi huo, aliyataja kuwa ni mradi umepunguza gharama za ununuaji wa gesi kutoka kg 800 hadi kg 400 kwa mwezi jambo lililookoa shilingi 12,000,000 kwa mwaka. Mafanikio mengine aliyataja kuwa mradi umesaidia kuweka mazingira katika hali ya usafi na kurahisisha utendaji kazi.

Nae mkazi wa Kata ya Iyumbu, Mussa Ipyana alisema kuwa maono ya rais kuhusu matumizi ya nishati safi yanatakiwa kuungwa mkono na watanzania wote.

Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa Mwaka 2026, Wazo Mwangónda alizindua mradi huo na kuishukuru serikali kwa uwekezaji mkubwa uliofanyika. Alisema kuwa mfumo wa nishati safi ya kupikia unapunguza gharama za upishi shuleni hapo. Aidha, aliishauri Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kusimika mfumo huo katika shule nyingine za sekondari.

Shule ya Sekondari Dr. Samia-Dodoma ilisajiliwa tarehe 05 Julai, 2023 sasa ina jumla ya wanafunzi 608, walimu 30 na wafanyakazi wasio walimu 09.

MWISHO

Comments

Popular Posts

Baraza la Madiwani Jiji la Dodoma lawafukuza kazi watumishi watatu na mmoja kushushwa cheo