Mwenge wa Uhuru 2026 wakabidhi gari la shilingi 121 Kikundi cha Vijana

Na. Dennis Gondwe, DODOMA

KIONGOZI wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa Mwaka 2026, Wazo Mwang’onda ametembelea na kukabidhi gari lenye thamani ya shilingi 121,871,152.50 fedha kutoka mapato ya ndani ya Halmashauri ya Jiji la Dodoma kupitia mkopo ya asilimia nne kwa kundi la vijana baada ya kujiridhisha na utendaji kazi wa Kikundi cha Mwamko wa Vijana Kiuchumi.



Tukio hilo lilifanyika katika Shule ya Sekondari Umonga baada ya kupokea taarifa ya Kikundi cha Mwamko wa Vijana Kiuchumi (MVK) na kushuhudia makala fupi ya safari na shughuli za kikundi.

Kiongozi wa Mwenge wa Uhuru Kitaifa Wazo Mwang’onda alisema kuwa utaratibu wa serikali kutoa mikopo isiyo na riba kwa vijana ni uamuzi bora. Lengo la mikopo hii ni kuwakomboa vijana kwa kuwapatia mitaji kwa ajili ya kuendesha biashara na kufanya shughuli za kujiongezea kipato. Aidha, aliwapongeza vijana hao kwa ubunifu wao katika kutekeleza majukumu yao.

Akisoma taarifa ya mradi wa Kikundi cha Mwamko wa Vijana Kiuchumi kinachojishughulisha na usafi wa mazingira kwa Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa Mwaka 2026, Mjumbe wa Kikundi, Bless Noel alisema kuwa lengo la mradi huo ni kujikwamua kiuchumi na kujipatia kipato kupitia shughuli za usafi wa mazingira na udhibiti wa taka ngumu katika Halmashauri ya Jiji la Dodoma.

Akiongelea mafanikio ya kikundi hicho, aliyataja kuwa ni kuweza kujiendesha, kutoa ajira za muda mrefu na mfupi kwa watu 25 wakiwemo madereva wa guta sita, wapakiaji taka 12, wakusanya fedha saba na kuanzisha mfumo wa kidijitali (App) utakao tusaidia mawasiliano na wateja ambao wanahitaji huduma za kuondolewa taka kwa haraka. “Kikundi kilipata habari ya uwepo wa fursa ya mkopo wa asilimia 10 hasa kundi la asilimia nne ya vijana. Mwezi Desemba, 2025 tulianza mchakato halmashauri, benki ya NMB walitutembelea na kupendekeza tupewe mkopo usio na riba wa shilingi 121,871,152.50. Fedha hizo za mkopo tumetumia kununua gari ya kubebea taka aina ya Tipper tani nane kwa shilingi 114,750,000, kulipa bima kubwa shilingi 5,754,712 na kuweka mfumo wa kufuatilia gari (Car tracker) 1,366,440. Gari hilo litatuwezesha kuwahudumia wateja 4,800 tulio watambua, kuongeza ufanisi wa kazi, na kupeleka dampo moja kwa moja” alisema Noel.




Kikundi cha Mwamko wa Vijana Kiuchumi kilisajiliwa mwaka 2020 kikiwa na wanakikundi watano kikianza kwa mtaji wa shilingi 300,000 fedha iliyotumika kukodi mkokoteni na kununua vifaa vya usafi na kuanza shughuli za ukusanyaji taka ngumu katika Mtaa wa Mbuyuni, Kata ya Kizota.

MWISHO

Comments

Popular Posts

Baraza la Madiwani Jiji la Dodoma lawafukuza kazi watumishi watatu na mmoja kushushwa cheo