Na. Dennis Gondwe, TAMBUKARELI
HALMASHAURI
ya Jiji la Dodoma imetumia shilingi 519,891,609 kwa ajili ya kusimika mfumo wa
kamera za usalama ili kuwahakikishia ulinzi na usalama wananchi na mali zao
pamoja na wawekezaji.
Kauli
hiyo ilitolewa na Mkuu wa Kitengo cha Teknolojia ya Habari na Mawasiliano
Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Joseph Fungo alipokuwa akiwasilisha taarifa ya
mradi wa kusimika kamera za usalama jijini Dodoma kwa Kiongozi wa Mbio za
Mwenge wa Uhuru Kitaifa Mwaka 2026 tukio lililofanyika katika Hoteli ya
Starline jijini Dodoma.
Akiongelea
lengo la mradi huo, alisema kuwa ni kuimarisha ulinzi na usalama wa wananchi na
mali zao. “Kamera hizi zinalenga kulinda miundombinu ya Umma katika Jiji la Dodoma,
kudhibiti makosa ya barabarani na matendo ya uhalifu. Aidha, mradi utasaidia
kutoa uhakika wa usalama kwa wadau wa shughuli za maendeleo
na kulifanya Jiji la Dodoma kuwa salama kwa shughuli za uwekezaji,
kidiplomasia, utalii na kuhakikisha Jiji linaendeshwa kidijitali” alisema
Fungo.
Akiongelea
gharama za mradi, alisema kuwa jumla ni shilingi 682,561,548. “Kati ya fedha hizo shilingi 519,891,609.27 zimetolewa na
Halmashauri ya Jiji la Dodoma kupitia mapato ya ndani na shilingi 162,669,939.34 zimetolewa na Mfuko wa
Mawasiliano kwa Wote nchini Tanzania (UCSAF) ambazo zitalipwa kwa Shirika la
Mawasiliano Tanzania (TTCL), taasisi inayotekeleza jukumu la kuunganisha mfumo
mzima wa kamera kupitia mkongo wa taifa” alisema Fungo.
Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa Wazo Mwang’onda aliipongeza
Halmashauri ya Jiji la Dodoma kwa kusimika kamera za usalama. Alisema kuwa
kutokana na usimikaji wa mfumo huo, usalama ni mkubwa na kuwahakikishia
wawekezaji kuwa watakuwa salama.
Alisema kuwa rai ya Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa wananchi wa Dodoma
ni kulinda na kutunza amani ya nchi. Alisema kuwa maendeleo hayawezi kufanyika
sehemu ambayo haina usalama na amani. “Mwenge wa Uhuru umetembelea mradi wa
kamera za usalama na umefurahishwa sana na mradi huu” alisema Mwang’onda.
Nae mkazi wa Kata ya Tambukareli, Neema Wande alisema kuwa kamera za
usalama zimesimikwa wakati muafaka ambapo Jiji la Dodoma linajitofautisha na
maeneo mengine katika eneo la matumizi ya teknolojia kwa usalama wa watu na
mali zao.
Mradi unatekelezwa na Kampuni ya Wisjane Smart Sytems ukiwa umefikia
asilimia 80 ya utekelezaji.
MWISHO
Comments
Post a Comment