Vijana watakiwa kuepuka matumizi ya Dawa za kulevya Dodoma

 

Na. Mwandishi wetu, DODOMA

VIJANA wahimizwa kuepuka matumizi ya dawa za kulevya ambayo yanatajwa kuwa na madhara makubwa ili kulinda afya zao na kuchangia maendeleo ya taifa.



Akizungumza katika Kongamano la Vijana lililofanyika katika ukumbi wa Chuo cha Mipango na Maendeleo Vijijini (IRDP), Afisa Mwandamizi kutoka Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya, Anna Tengia alisema kuwa dawa za kulevya ni kemikali zinazobadilisha mfumo wa fahamu wa binadamu na kuathiri mtu anavyofikiri na kutenda.

Aliweka mkazo kuwa vijana wajilinde ili kujenga kizazi imara na kinachofikiria mustakabali bora wa maisha yao. “Dawa za kulevya huathiri afya ya akili na mwili wa mtumiaji. Kwa maana hiyo hupunguza uwezo wa vijana kushiriki kikamilifu katika shughuli za maendeleo” alisema Tengia.

Kwa upande wake, Afisa Sheria wa mamlaka hiyo, Meshak Lyabonga wakati akitoa elimu alisisitiza kuwa matumizi ya dawa za kulevya ni kosa la kisheria na wahusika wanaweza kuchukuliwa hatua kwa mujibu wa sheria.

Kongamano hilo limeonesha umuhimu wa vijana kukutana na kufanya mijadala muhimu ambayo itawasaidia katika kufanya maamuzi sahihi ili kuepuka matumizi ya dawa za kulevya na kulinda afya zao.






MWISHO

Comments

Popular Posts

Baraza la Madiwani Jiji la Dodoma lawafukuza kazi watumishi watatu na mmoja kushushwa cheo

Odero: Mwenge wa Uhuru alama ya Umoja Wilayani Dodoma