Jamii yatakiwa kuwajengea watoto utamaduni wa kupenda kupanda Miti na kuhifadhi Mazingira
Na. Dennis Gondwe, DODOMA
WADAU wa uhifadhi wa Mazingira wametakiwa kuwajengea
watoto utaratibu wa kupanda miti na kupenda kudumisha usafi wa Mazingira katika
maeneo yanayowazunguka ili kuwa na mandhari nzuri ya kuvutia.
Kauli hiyo ilitolewa na Katibu Tawala Mkoa wa Dodoma, Dkt. Khatibu Kazungu alipomuwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Dodoma katika zoezi la usafi wa Mazingira ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya Siku ya Mazingira Duniani lililofanyika katika Soko la wazi la Machinga jijini Dodoma.
Akizungumza na mamia ya wananchi waliojitokeza
kushiriki zoezi hilo la usafi, alisema kuwa wadau wa masuala ya usafi na jamii
kwa ujumla wana wajibu wa kuwafundisha na kuwarithisha watoto kupenda usafi na
kuchukia mazingira machafu. “Pamoja na usafi, pia tuwakumbushe watoto wetu
kupanda miti katika maeneo yanayotuzunguka. Kurithisha tabia ya kupenda kupanda
miti inatuhakikishia mandhari nzuri inayotuzunguka na kuepuka tishio la mabadiliko
ya tabia nchi” alisema Dkt. Kazungu.
Kwa upande wake, mwakilishi wa Mkurugenzi Msaidizi wa
Mazingira kutoka Ofisi ya Makamu wa Rais- Muungano na Mazingira, Martha
Ngalowera alisema kuwa zoezi la usafi wa mazingira katika Soko la wazi la Machinga ni kuweka alama ya maadhimisho ya Siku
ya Mazingira Duniani.
Alisema kuwa maadhimisho hayo yanaongozwa na kaulimbiu
isemayo ‘Dira 2050, tuwajibike kukijanisha Tanzania’. “Kupitia kaulimbiu hii tunatarajia
ifikapo Mwaka 2050, Tanzania iwe kati ya nchi 10 bora katika uhifadhi wa
mazingira. Kwa maana hiyo, kaulimbiu hii inalenga kuhamasisha jamii kuelekea
Dira 2050” alisema Ngalowera.
Ikumbukwe kuwa maadhimisho ya Siku ya Mazingira Duniani nchini yalianza tarehe 11 Mei na yanatarajiwa kuhitimishwa tarehe 5 Juni, 2026, baada ya Waziri mwenye dhamana na Mazingira kutoa tamko rasmi la serikali la maadhimisho ya Siku ya Mazingira Duniani, yatakayokuwa pamoja na mambo mengine kuzindua programu kabambe ya kukijanisha Tanzania ikilenga kuifanya kuwa kinara wa uhifadhi wa Mazingira.
Comments
Post a Comment