Vijana Dodoma watakiwa kutekeleza wajibu wao katika jamii
Na. Mwandishi Wetu, DODOMA
VIJANA wametakiwa kujitambua, kuthamini nafasi yao
katika maendeleo ya taifa na kutekeleza wajibu kwa familia na jamii kwa ujumla
ili kuchangia ustawi wa nchi.
Wito huo ulitolewa na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Patrobas Katambi wakati akizungumza katika Kongamano la Vijana lililofanyika katika ukumbi wa Chuo cha Mipango na Maendeleo Vijijini (IRDP) katika Wilaya ya Dodoma ikiwa ni kuelekea mapokezi ya Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa Mwaka 2026 katika ya Wilaya ya Dodoma.
Alisema kuwa vijana wana nafasi kubwa katika kuendeleza
amani, uzalendo na maendeleo ya taifa, hivyo wanapaswa kutumia fursa walizonazo
kwa manufaa yao na ya jamii inayowazunguka. “Kuelekea Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa
Mwaka 2026, ninawahimiza vijana wote kujitambua, kujua wajibu wao kwa familia,
jamii na taifa kwa ujumla. Vijana ndiyo nguvu kazi ya taifa na msingi wa
maendeleo endelevu” alisema Katambi.
Aliongeza kuwa Mwenge wa Uhuru unaendelea kuwa chombo
muhimu cha kuhamasisha maendeleo, kudumisha umoja wa kitaifa na kuibua miradi
yenye manufaa kwa wananchi, hivyo ushiriki wa vijana katika shughuli zake ni
jambo la msingi.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Dodoma, Alhaj Jabir
Shekimweri alitoa shukrani kwa waziri kuweza kushiriki katika kongamano hilo. “Kwanza
kabisa nitoe pongezi zangu za dhati kwa waziri ambapo ameweza kuungana na sisi
katika kongamano hili na kutoa nasaha zake na kuzungumza na vijana wa Wilaya ya
Dodoma. Hivyo, nina imani kupitia mafunzo haya vijana hawa wataenda kuwa bora”
alisema Alhaj Shekimweri.
Kongamano hilo lililenga kujadili nafasi ya vijana
katika maendeleo ya taifa, kujenga uzalendo na kuhamasisha ushiriki wao katika
shughuli mbalimbali za kijamii na kiuchumi kuelekea Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa
Mwaka 2026 itakayofanyika tarehe 1 Juni, 2026.
MWISHO
Comments
Post a Comment