Waziri Mkuu amtaka Mkandarasi kukamilisha Soko Kuu la Majengo kwa wakati

Na. Nancy Kivuyo, DODOMA

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mwigulu Nchemba atembelea Soko Kuu la Majengo jijini Dodoma leo kwa ajili ya kukagua maendeleo ya ukarabati wa soko hilo na kutoa maagizo kwa mkandarasi anayekarabati soko hilo kuhakikisha kazi inakamilika kwa wakati na kwa ubora unaostahili.





Katika ziara hiyo, Waziri Mkuu aliambatana na viongozi wa Mkoa wa Dodoma pamoja na Halmashauri ya Jiji la Dodoma ambapo alisomewa taarifa ya ukarabati wa miundombinu mbalimbali inayoboreshwa kama vile maeneo ya biashara, mitaro ya maji ya mvua, mifumo ya usalama na umeme.

Baada ya taarifa hiyo, Waziri Mkuu alisema kuwa serikali imejipanga kuhakikisha soko linarejea katika matumizi haraka ili kuwezesha wananchi na wafanyabiashara kunufaika na miundombinu bora. “Mradi huu ni muhimu sana kwa wananchi wa Dodoma na lazima ukamilike kwa wakati na kwa kiwango bora. Mkandarasi hakikisha soko hili linakamilika kama ambavyo mkataba unasema. Nanyi jiji naelekeza kuwa soko litakapokamilika hawa wafanyabiashara waliokuwa hapo ndio wapewe kipaumbele na sio vinginevyo. Tunatarajia kuwa mtasimamia vizuri pasiwepo malalamiko” alisema Dkt. Nchemba.

Nae, Mbunge wa Jimbo la Dodoma Mjini, Paschal Chinyele ambaye alihudhuria ziara hiyo, alimkaribisha Waziri Mkuu na kueleza kuwa wafanyabiashara wanasubiri kwa hamu kukamilika kwa soko hilo ili warejee kuendelea na shughuli zao. “Wafanyabiashara wetu wanategemea soko hili kwa kipato chao cha kila siku. Wamevumilia kipindi cha ukarabati na wanaomba likamilike kwa wakati. Pia baadhi ya barabara zimefungwa kupisha ukarabati, hivyo wananchi wana matarajio makubwa” alisema Chinyele.



Aidha, mbunge huyo aliiomba serikali kuangalia uwezekano wa kujenga maegesho ya magari katika eneo la korongo lililopo pembezoni mwa soko ili kuboresha zaidi mandhari na uendeshaji wa shughuli za kila siku. “Eneo lile lina nafasi nzuri kwa maegesho ya kisasa ambayo yatapunguza msongamano na kuongeza mpangilio mzuri wa biashara na soko letu kwa ujumla” aliomba Chinyele.

Katika hatua nyingine mfanyabiashara wa Soko la Majengo, Rose Mtundu aliipongeza serikali kwa jitihada za kuboresha soko hilo. “Tunashukuru kuona serikali inafuatilia ukarabati huu kwa karibu. Soko likikamilika litakuwa msaada mkubwa kwa wananchi na sisi wafanyabiashara. Tunatarajia patakuwa sehemu salama na penye mpangilio” alisema Mtundu.

Ziara hiyo imeonesha matumaini makubwa ya wananchi na viongozi kwamba Soko Kuu la Majengo litakuwa miongoni mwa masoko ya kisasa na yenye kutoa fursa pana za kiuchumi kwa wakazi wa Dodoma.

MWISHO

Comments

Popular Posts

Watumishi wa Kanda Namba Tatu watembelea Zahanati ya Soweto

Gari la Darasa Tembezi latoa elimu Mitaa ya Jiji la Dodoma