Diwani Alimwoni Chaula, achaguliwa Meya Jiji la Dodoma
Na. Dennis Gondwe, DODOMA
Baraza
la Madiwani la Halmashauri ya Jiji la Dodoma katika mkutano wake wa kwanza
limemchangua Alimwoni Simon Chaula, Diwani wa Kata ya Makutupora kuwa Mstahiki
Meya wa Jiji hilo kwa kupata kura za ndiyo 57 sawa na asilimia 100 ya kura zote
zilizopigwa.
Akitangaza matokeo ya kura zilizopigwa, Mwenyekiti wa Mkutano wa Halmashauri, Sakina Mbugi alitangaza kuwa Diwani Alimwoni Chaula alipata kura 57 kati ya kura 57 zilizopigwa na wajumbe. “Niwapongeze wajumbe wote halali mlioshiriki kupiga kura kwa nafasi ya Mstahiki Meya na Naibu Meya. Naomba kutanga za matokeo kama ifuatavyo. Nafasi ya Mstahiki Meya, kura 57 zilipigwa, hakuna kura ambayo haikupigwa. Kura zote 57 ni kura za ndiyo. Kwa matokeo hayo, ninamtangaza rasmi Mheshimiwa Alimwoni Chaula kuwa Mstahiki Meya wa Jiji la Dodoma. Nafasi ya Naibu Meya, jumla kura zilizopigwa 55 kati ya kura 57. Wajumbe wawili hawakupiga kura. Kura za ndiyo ni zote 55. Hivyo, ninatangaza rasmi kuwa Mheshimiwa Bakari Fundikira ameshinda uchaguzi na amekuwa Naibu Meya wa Jiji la Dodoma. Hongera sana” alisema Mbugi.
Awali
akiomba kura katika mkutano huo, Alimwoni Chaula alisema kuwa aliomba nafasi
hiyo kwa sababu anao uwezo na ari ya kuitumikia halmashauri. “Nitashirikiana
sana na wafanyakazi wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma, nitashirikiana sana na
madiwani wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma kufanikisha ile dhima ya rais wetu,
ya kazi na utu mbele. Nawaomba madiwani wenzangu kura za ndiyo, naomba tumalize
kwa haki” alisema Chaula.
Katibu
wa Mkutano wa kwanza wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Dkt. Frederick Sagamiko
alisema kuwa baada ya uchaguzi mkuu, kata zote na madiwani wa viti maalum
ushindi ulienda kwa Chama Cha Mapinduzi. Hivyo basi, katika uchaguzi huu
tutakuwa na wawakilishi wa chama kimoja ambacho ni CCM. Tarehe 2 Desemba, 2025
nilipokea barua kutoka kwa Katibu wa CCM Wilaya ya Dodoma kuwasilisha jina la
Mstahiki Meya na jina la Naibu Meya wa Jiji la Dodoma ili kuendelea na taratibu
za kiserikali. “Alimwoni Simon Chaula amependekezwa kupombea nafasi ya Mstahiki
Meya na Bakari Samwel Fundikira amependekezwa kugombea nafasi ya Naibu Meya wa
Jiji la Dodoma” alisema Dkt. Sagamiko.
MWISHO
Comments
Post a Comment