Madiwani watakiwa kuifanya Dodoma kuwa kinara ukusanyaji mapato
Na. Dennis Gondwe, DODOMA
MKUU wa Wilaya ya Dodoma, Alhaj Jabir Shekimweri
amelitaka Baraza la Madiwani kuendelea kuifanya Halmashauri ya Jiji la Dodoma
kuwa kinara katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo kupitia mapato ya ndani
ili kuwaletea wananchi maendeleo na kuboresha maisha yao.
Kauli hiyo aliitoa alipokuwa akiwasalimia madiwani
katika mkutano wa kwanza wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma uliofanyika katika
ukumbi wa halmashauri jijini hapa.
Alhaj Shekimweri alisema “katika mapato ya ndani
mmekuwa vinara katika kutekeleza miradi mizuri
ya maendeleo. Tumeona miradi ya hoteli, mradi wa Soko la wazi la
Machinga, miradi ya ujenzi wa barabara, mfano ile ya Nala kuelekea hospitali ya
jiji na miradi mingine mingi. Nendeni mkawe vinara wa kutekeleza miradi ya
maendeleo. Ninayasema haya kwa kumuenzi Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwamba
mnapochukua madaraka yale mema yaliyoanzishwa na wenzenu msiyaweke kando,
ambayo hayajakamilika mkayakamilishe, yanayoendelea mkayakalishe huku
mkianzisha mengine mapya”.
Nae, Mkurugenzi wa Jiji la Dodoma alisema kuwa jiji
lilikusanya jumla ya shilingi bilioni 22, 193,124,132.17 kwa kipindi cha Julai – Oktoba ambayo ni sawa
na asilimia 30.9 ya lengo la mwaka.
Katika hatua nyingine, Diwani wa Kata ya Dodoma
Makulu, Samson Mkopi alipongeza makusanyo yaliyopatikana na kuahidi
kushirikiana na watendaji katika kanda ili kuongeza mapato. “Ndugu Mwenyekiti,
tunapongeza sana makusanyo hayo, ni imani yetu kuwa tutatoa ushirikiano zaidi
ili kuongeza ukusanyaji mkubwa wa mapato katika jiji letu ili mapato ya ndani
yaweze kwenda kwa wananchi kutekeleza miradi ya maendeleo” alipongeza.
MWISHO
Comments
Post a Comment