Madiwani Jiji la Dodoma watakiwa kuwa walezi
Na. Dennis Gondwe, DODOMA
MADIWANI wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma wametakiwa
kutumia nafasi yao na kuwa walezi kwa maafisa watendaji katika kata zao na
kuwasimamia ili kuwaletea maendeleo wananchi.
Rai hiyo ilitolewa na Mkuu wa Wilaya ya Dodoma, Alhaj Jabir Shekimweri alipokuwa akiongea na madiwani katika mkutano wa kwanza wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma baada ya Uchaguzi Mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani wa tarehe 29 Oktoba, 2025.
“Waheshimiwa Madiwani, nataka niwaombe sana mkawalee
maafisa watendaji wenu kwenye ngazi ya kata. Mstahiki Meya, ninasema hapa kwa
kuwaangukia na kuwaomba, mkawe walezi, ninyi ndiyo wenyeviti wa kamati za
maendeleo kwenye kata, mkono wako wa kulia ni katibu, ambae ni Afisa Mtendaji
wa Kata. Watendaji hawa inawezekana wakawa na madhaifu ya hapa na pale, nenda
ukawe mlezi, nenda ukawe mzazi, yeye pamoja na wataalam wengine ngazi ya kata.
Wasaidieni wafanye majukumu yao sawasawa ili wewe upate matokeo na kuwaletea
wananchi maendeleo. Mimi, nitakusifu sana ukimkuta mtendaji ambae
anachangamoto, ukamsaidia akaimarika kwenye changamoto yake, akawa mtendaji
mzuri. Hivyo, kila mmoja akija hapa na kulalamika huyu mtendaji siyo mzuri,
tumtoe, siyo mzuri mtoe, namtoa nampeleka wapi?, Nataka niwaombe sana, hata
sisi wenyewe hatujakamilika…twende tukawajenge wafanye kazi zao vizuri ili
watusaidie katika majukumu yetu kwenye kata zetu” alisema Alhaj Shekimweri.
MWISHO
Comments
Post a Comment