Madiwani Jiji la Dodoma watakiwa kutoa tamko la rasilimali na madeni
Na. Dennis Gondwe, DODOMA
SEKRETARIETI ya Maadili ya Viongozi wa Umma imewataka
madiwani wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma kutoa tamko la rasilimali na madeni
kwa mujibu wa sheria.
Kauli hiyo ilitolewa na Katibu Msaidizi Kanda ya Kati, Ofisi ya Rais, Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma, Jasmin Bakari wakati akiwaongoza kutoa tamko la kimaandishi la ahadi ya uadilifu kwa viongozi wa umma katika ukumbi wa mikutano wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma.
“Niwapongeze kwa kufanikiwa kuchaguliwa kuwa madiwani,
ni mategemeo yetu mtatekeleza majukumu yenu kwa viwango vya juu vya maadili, na
mviishi viapo vyenu. Niwakumbushe madiwani na viongozi wote waliopo hapa kutoa
tamko la rasilimali na madeni, tunawakumbusha kuingia kwenye mfumo kwa wale
wapya kuna sehemu ya kujisajili. Kwa wale waliokuwa baraza lililopita wataingia
kwa akaunti zao za awali” alisema Bakari.
Nae, Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya
Dodoma, Charles Mamba aliiomba kamati ya maadili ianze kazi mapema ili kuondoa
makundi na chuki. “Katibu, nashauri kwamba kamati ya madili ianze kufanya kazi
mapema iwezekanavyo. Tuna matarajio na uwepo wenu katika baraza hili.
Saidianeni ili kuvushana katika utendaji kazi” alisema Mamba.
Alimalizia kusema kuwa, madiwani watumie weledi katika
kufuatilia utekelezaji wa miradi ya maendeleo ili wananchi wanufaike moja kwa
moja.
Katika hatua nyingine, Diwani wa Kata ya Mpunguzi,
Isaya Chilongani alipongeza uundwaji wa baraza na kuahidi kutoa ushirikiano
katika utendaji kazi. “Namshukuru sana Mwenyezi Mungu kwa siku ya leo, kuanza
rasmi kwa baraza hili ni ishara kuwa tuna nafasi kubwa sana ya kuwatumikia
wananchi. Nipo tayari kutoa ushirikiano kwa madiwani wenzangu na wananchi ili kufanikisha
lile lengo la kuleta maendeleo katika kata zetu” alipongeza Chilongani.
MWISHO
Comments
Post a Comment